1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Marekani yasusia kutoa heshima kwa hayati Raisi

31 Mei 2024

Marekani na mataifa mengine ya Magharibi yamegoma kuhudhuria hafla ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kutoa heshima kwa Rais wa Iran Ebrahim Raisi aliyekufa katika ajali ya helikopta Mei 19.

https://p.dw.com/p/4gUWH
Kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kutoa heshima kwa aliyekuwa rais wa Iran, hayati Ebrahim Raisi.
Kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kutoa heshima kwa aliyekuwa rais wa Iran, hayati Ebrahim Raisi 30.05.2024Picha: Kena Betancur/AFP

Marekani imesusia kutoa heshima za Umoja wa Mataifa kwa Rais wa Iran Ebrahim Raisi siku ya Alhamisi (30.05.2024) kwa sababu ilisema alihusika katika matukio mengi ya ukiukwaji wa kutisha wa haki za binadamu na kwamba chombo hicho cha kimataifa kinapaswa badala yake kisimame na watu wa Iran.

Nante Evans, msemaji wa ujumbe wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amesema Marekani haingehudhuria hafla hiyo ya kumuenzi Rais Raisi katika nafasi yoyote ile. Nante alisema Raisi alihusika katika vitendo kadhaa vya kutisha vya ukiukaji wa haki za binadamu na unyanyasaji, ikiwa ni pamoja na mauaji ya maelfu ya watu kinyume cha sheria na wafungwa wa kisiasa mnamo mwaka 1988. Nante pia amesema baadhi ya matukio mabaya kabisa ya ukiukaji wa haki za binadamu kuwahi kurekodiwa yalifanyika wakati wa uongozi wake.

Ujumbe wa Iran katika Umoja wa Mataifa umekataa kutoa kauli kuhusu hatua ya Marekani.

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 193 kwa kawaida hukutana kutoa heshima kwa kiongozi yoyote wa dunia ambaye alikuwa mkuu wa nchi wakati wa kifo chake. Hotuba zilitolewa na nchi na makundi mbalimbali ya kikanda wakati wa kumbukumbu ya dakika 50 kwa hayati Raisi.

Guterres ahimiza ushirikiano wa kimataifa

Katika taarifa fupi katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameliambia baraza kuu la Umoja wa Mataifa kwamba katika nyakati hizi ngumu ushirikiano wa kimataifa na kikanda unahitajika zaidi kuliko awali na ushirikiano huo ni muhimu kujenga hali ya kuaminiana, kuepusha mizozo na kusuluhisha migogoro.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres akitoa heshima kwa hayati Ebrahim Raisi
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres akitoa heshima kwa hayati Ebrahim Raisi (pichani) 30.05.2024Picha: Kena Betancur/AFP

"Raisi aliiongoza Iran wakati wa kipindi cha changamoto kwa nchi hiyo, eneo la Mashariki ya Kati na ulimwengu mzima kwa ujumla. Guterres aidha amesema Umoja wa Mataifa unasimama kwa mshikamano na Wairan na katika kutafuta amani, maendeleo na uhuru msingi."

Soma pia: Iran yamzika Ebrahim Raisi eneo takatifu zaidi la Kishia

Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa Amir Saeid Iravani alizungumzia athari kubwa ya kifo cha Raisi na waziri wa mambo ya nje wa Iran Hossein Amirabdollahian, ambaye pia alikufa katika ajali hiyo ya helikopta. Iravani ameliambia baraza kuu la Umoja wa Mataifa kwamba kwa wakati huu wanatafakari athari za vifo vya viongozi hao kwa maisha yao na nchi yao.

"Hawakuwa tu viongozi waliokuwa na mamlaka bali pia nembo ya matumaini, uthabiti na nguvu ya kudumu ya utawala bora na diplomasia. Iravani pia alisema wanabaki na nia thabiti ya kuzingatia kanuni za amani, usalama, haki na ushirikiano wa pande mbalimbali ambao viongozi waliokufa waliuunga mkono bila kuchoka."

Raisi, ambaye alionekana kama mtu mwenye uwezo wa kumrithi Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, alikufa katika ajali ya helikopta iliyosababishwa na hali mbaya ya hewa katika milima iliyo karibu na mpaka wa Azabajani mnamo Mei 19. Uchaguzi wa urais kujaza pengo lililowachwa na Raisi umepangwa kufanyika Juni 28.

(afpe, reuters, ap)