Marekani yaiwekea vikwazo Mahakama ya ICC
7 Februari 2025Amri ya Rais Donald Trump ya kuiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC imetolewa Alhamisi ikikishutumu chombo hicho kwa kujihusisha na vitendo visivyo na msingi vilivyo kinyume cha sheria dhidi ya Marekani na Israel.
Zaidi, maelezo katika amri hiyo yameilaumu ICC kwa kutumia vibaya mamlaka yake dhidi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa kutoa waranti wa kukamatwa kwake pamoja na aliyekuwa Waziri wake wa Ulinzi, Yoav Gallant.
ICC ilitoa waranti wa kukamatwa kwa wawili hao ikiwatuhumu kwa kuhusika na uhalifu wa kivita kutokana na namna walivyojibu mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7 mwaka 2023. Hata Hivyo, Netanyahu amekuwa akiulalamikia uamuzi huo wa ICC akisema kuwa haukuwa wa haki.
Soma zaidi: Umoja Ulaya waahidi kuwa pamoja na ICC baada ya vikwazo vya Marekani
Amri maalumu iliyosainiwa na Trump dhidi ya ICC Alhamisi imeeleza kwamba Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu haina mamlaka juu ya Marekani na Israel ikizingatiwa kuwa nchi hizo mbili haziitambui mahakama hiyo.
Vikwazo vilivyowekwa na Marekani kupitia amri ya rais dhidi ya ICC vinaweza kujumuisha kuzuia mali na wafanyakazi wa mahakama hiyo pamoja na ndugu zao kuingia Marekani.
Israel yaupongeza uamuzi wa Trump
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Israel, Gideon Saar kupitia ukurasa wake wa X, ameipongeza hatua hiyo ya Trump akisema vitendo vya ICC vilikuwa sawa na uovu na havikufuata sheria.
Mahakama ya ICC kwa upande wake, imelaani amri ya Trump na imeapa kuwa itaendelea kutoa haki na matumaini kwa mamilioni ya watu wanaoathiriwa na ukatili kote duniani. Taarifa ya mahakama hiyo imesema kuwawekea vikwazo maafisa wake kunalenga kuharibu kazi ya mahakama huru isiyo na upendeleo.
Nao Umoja wa Ulaya, leo Ijumaa umeonya kuwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya ICC vinatishia uhuru wa chombo hicho na mfumo wa sheria.
Halmashauri ya umoja huo katika tamko tofauti limeilaani pia hatua hiyo na kutahadharisha kwamba amri dhidi ya ICC inaweza kuathiri upelelezi na kesi zinazoendelea zikiwemo zinazohusu Ukraine, na kuathiri juhudi za miaka mingi za kuhakikisha kunakuwa na uwajibikaji kote duniani.