1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
TeknolojiaMarekani

Marekani, Uingereza zaituhumu China kwa ujasusi wa mtandaoni

26 Machi 2024

Maafisa wa Marekani na Uingereza wamefungua mashitaka, kutangaza vikwazo, na kuituhumu China kwa kuendesha kampeni kubwa ya ujasusi wa mtandaoni.

https://p.dw.com/p/4e765
Udukuzi wa mtandaoni
Marekani na Uingereza zimesema ujasusi wa mtandaoni wa China umewakumba mamilioni ya watu Picha: picture alliance/dpa

Maafisa wa Marekani na Uingereza wamefungua mashitaka, kutangaza vikwazo, na kuituhumu China kwa kuendesha kampeni kubwa ya ujasusi wa mitandaoni ambayo inadaiwa kuwakumba mamilioni ya watu wakiwemo wabunge, wasomi, na waandishi habari, na makampuni wakiwemo wanakandarasi wa sekta ya ulinzi.

Maafisa kutoka pande zote mbili za Bahari ya Atlantiki walilipatia kundi hilo la udukuzi jina la utani la Advanced Persistent Threat 31 au APT31, wakiliita tawi la Wizara ya China ya Usalama wa Taifa. Naibu Mwanasheria Mkuu wa Marekani Lisa Monaco amesema katika taarifa kuwa lengo la operesheni hiyo ya udukuzi wa kimataifa lilikuwa ni "kuwakandamiza wakosoaji wa utawala wa China; kuingilia taasisi za serikali, na kuiba siri za biashara.

Soma pia: Harakati za kijasusi za Urusi kuongezeka nchini Ujerumani

Maafisa mjini London wameituhumu APT31 kwa kuwadukua wabunge wa Uingereza wanaoikosoa China na kusema kuwa kundi la pili la majasusi wa China lilihusika na udukuzi wa taasisi ya mausala ya uchaguzi ya Uingereza na kuingilia data za mamilioni ya watu nchini humo.

Wanadiplomasia wa China nchini Uingereza na Marekani wamepuuzilia mbali madai hayo wakisema hayana uhalali. Ubalozi wa China mjini London uliyaita mashitaka hayo kuwa ni "ya kutungwa kabisa na ni kashfa zenye nia mbaya."