1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Ulaya: Muafaka juu ya Iran bado upo mbali

24 Mei 2018

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amesema bado pana tofauti kubwa kati ya nchi yake na Marekani juu ya mkataba wa nyuklia wa Iran baada ya mazungumzo na mwenzake wa Marekani Mike Pompeo.

https://p.dw.com/p/2yEhW
USA Besuch Außenminister Heiko Maas, SPD in Washington
Picha: Imago/photothek

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani ametoa tathmini yake baada ya kukutana na waziri mwenzake wa Marekani Mike Pompeo, ambapo amesema wote walisisitiza misimamo ya nchi zao kuhusu mkataba wa nyuklia wa Iran. Nchi za Ulaya zimo katika hali ya kutoelewana na Marekani tangu Rais Donald Trump alipochukua hatua ya kuiondoa nchi yake kwenye mkataba huo wa nyuklia uliofikiwa na Iran mwaka 2015. Waziri Heiko Maas amesema hakuna hatua zozote mpya zilizofikiwa kwenye mazungumzo yao.

Naye waziri wa mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian, amesema mbinu za Marekani zinaweza kuitumbukiza Mashariki ya Kati kwenye migogoro zaidi na kwamba vikwazo vipya dhidi ya Iran havitasabisha majadiliano yafanyike bali kinyume chake, vitaongeza umuhimu na nguvu ya wahafidhina wa Iran na wakati huo huo kumdhoofisha rais Hassan Rouhani, ambaye yuko tayari kujadiliana.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Mike Pompeo
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Mike PompeoPicha: picture-alliance/AP Photo/J. S. Applewhite

Marekani hivi karibuni ilijitoa kwenye mkataba huo na kuiwekea Iran vikwazo vipya. Mbali na hayo bwana Maas amesema walijadiliana pia kuhusu mgogoro wa Syria na hali kwa jumla katika Mashariki ya Kati pamoja na mivutano ya kibiashara inayoendelea kati ya Marekani na nchi nyingine.

Wakati huo huo Utawala wa raisTrump umeanzisha uchunguzi juu ya uagizaji wa magari na malori ambao unaweza kusababisha nyongeza ya kodi kama ushuru mpya ulioanzishwa mwezi Machi kwa bidhaa za chuma na bati zinazoingizwa nchini Marekani.

Waziri wa biashara wa Marekani Wilbur Ross amesema uagizaji wa magari kutoka nje ya Marekani kwa miongo kadhaa umezorotesha sekta ya utengenezaji magari ya ndani ya nchi hiyo. Waziri Ross ameahidi kwamba uchunguzi huo wa kina utafanyika kwa haki na uwazi.

Ujerumani na Asia zitaathirika iwapo Marekani itaamua kuongeza kodi za magari yatakayoingizwa nchini mwake. Kampuni za kutengeneza magari za Ujerumani Volkswagen, Daimler na BMW zina viwanda vikubwa vya kuunganisha magari nchini Marekani. Ujerumani ni ya pili katika kupeleka bidhaa nchini Marekani baada ya China na mauzo ya magari pamoja na vipuri ndio chanzo kikubwa cha mapato ya nje kwa Ujerumani.

Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE/RTRE.

Mhariri: Iddi Ssessanga