1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na China zaanza duru mpya ya mazungumzo

31 Januari 2019

Duru nyingine ya mazungumzo juu ya kuutatua mgogoro wa kibiashara baina ya Marekani na China inaanza hii leo Alhamisi. Wajumbe wa ngazi za juu wa kutoka nchi mbili hizo wanakutana mjini Washington.

https://p.dw.com/p/3CTrj
USA China Gespräche im Handelskonflikt
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Harnik

Wajumbe hao wanatarajiwa kutafuta njia za kuepusha kupanuka kwa mgogoro huo wa kibiashara kati ya nchi mbili hizo. Marekani na China zimebakiwa na mwezi mmoja hadi mwisho wa muda wa siku 90 walizokubaliana mnamo mwezi Desemba mwaka uliopita, kusimamisha mvutano wa kibiashara baina yao.

Ikiwa mazungumzo hayo hayatafanikiwa, itakapofika tarehe 2 Machi, Marekani itaziongezea ushuru wa thamani ya dola bilioni 200 bidhaa kutoka China. Wachumi wanahofia kwamba mvutano huo unaweza kusababisha athari kubwa katika uchumi wa dunia. Juu ya mgogoro huo wa kibiashara kamishna wa idara ya takwimu wa China Ning Jizhe amesema mgogoro huo wa biashara unaathiri uchumi wa China huku Marekani ikikiri kuwa uchumi wake umeathirika kutokana na mgogoro huo .

Kiongozi wa ujumbe wa watu 30 kutoka Beijing, ambaye ni makamu wa rais wa China Liu He alimweleza mwakilishi wa biashara wa Marekani kwenye mazungumzo hayo, Robert Lighthizer juu ya kutofurahishwa na hatua ya kufunguliwa mashtaka kampuni kubwa ya mawasiliano ya China Huawei hatua ambayo amesema ni kinyume cha sheria. Hatua hiyo huenda ikayavuruga mazungumzo ya biashara kati ya nchi mbili hizo. Marekani na China nchi zenye nguvu kubwa za kiuchumi duniani zinapigania udhibiti wa baadaye katika sekta muhimu ya teknolojia.

Waziri wa fedha wa Marekani Steven Mnuchin
Waziri wa fedha wa Marekani Steven Mnuchin Picha: Reuters/J. Young

Miaka mitatu iliyopita, China ilizindua mpango wa kimkakati unaoitwa "Bidhaa za China kufikia mwaka 2025" ambao unalenga kulifanya taifa hilo kuwa kiongozi wa kimataifa katika uhandisi wa teknolojia ya anga, matumizi ya maroboti, utengenezaji wa mashine zenye kutumia teknolojia ya akili ya bandia, ubunifu mpya katika utengenezaji wa magari na maeneo mengine yanayohusiana na teknolojia ya kisasa, sekta ambayo Marekani inasema ni eneo la taifa hilo kubwa ambalo linaamini kuwa linaongoza katika masuala ya teknolojia, ubunifu na uvumbuzi.

Rais wa Marekani Donald Trump amesema mara kwa mara kwamba sio haki kwa uchumi wa China kuendelea kukua kwa gharama ya biashara na ujuzi wa Marekani. Nchi hiyo inailaumu China kwa kutokuzingatia haki katika biashara, kutokana na wizi wa hati fungani za raia wa Marekani na vitendo vya udukuzi wa teknolojia.

Ili kuishinikiza China, Marekani imeitoza nchi hiyo ushuru wa dola bilioni 250 kwa bidhaa zake zinazoingia Marekani. Kwa upande wake China inazitoza ushuru wa dola bilioni 110 bidhaa zinazotoka Marekani.

Waziri wa fedha wa Marekani Steven Mnuchin amesema kutokana na ugumu wa masuala hayo, makubaliano ya kuumaliza mgogoro huo hayatazamiwi kufikiwa kwenye mkutano huo wa siku mbili wa mjini Washington lakini anatarajia watapiga hatua kubwa.

Mwandishi:Zainab Aziz/AFPE

Mhariri:Gakuba, Daniel