1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini italipa gharama ikiipa silaha Urusi

Josephat Charo
6 Septemba 2023

Marekani imeonya kwamba Korea Kaskazini italipa gharama iwapo itaipekea silaha Urusi kwa ajili ya vita nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/4Vzce
Jake Sullivan
Picha: Kevin Lamarque/REUTERS

Ikulu ya Marekani imetahadharisha kwamba Korea Kaskazini italipa gharama iwapo itaipelekea silaha Urusi kwa ajili ya vita vyake nchini Ukraine. Tahadhari hiyo imetolewa huku kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un na rais wa Urusi Vladimir Putin wakitarajiwa kukutana kwa ajili ya mazungumzo.

Jake Sullivan, mshauri wa usalama wa taifa wa rais wa Marekani Joe Biden amesema Korea Kaskazini na Urusi zinapania kufanya mazungumzo katika ngazi ya viongozi wao pengine hata ya ana kwa ana kuhusu mahitaji ya sialaha ya Urusi.

Sullivan amesema Urusi huenda ikazitumia silaza kutoka Korea Kaskazini kushambulia shehena za vyakula katika maghala ya nafaka na miundombinu ya kupasha joto majumbani kuelekea msimu wa baridi kujaribu kuyateka maeneo ambayo ni himaya ya nchi nyingine huru.

"Hii haitatoa picha nzuri kwa Korea Kaskazini na watalipa gharama kwa hatua hii katika ngazi ya jumuiya ya kimataifa," aliongeza kusema Sullivan.

Sullivan aliongeza kwamba "hatua hii inasema mengi kuhusu Urusi kulazimika kuigeukia nchi kama Korea Kaskazini".

Ikulu ya Marekani imesema waziri wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu alisafiri kwenda Korea Kaskazini mwezi Julai mwaka huu akitafuta kupata silaha za nyongeza kwa ajili ya vita.

Utawala wa Kremlin umesema hauwezi kuthibitisha taarifa kuhusu mkutano wa kilele kati ya Putin na Kim.