1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mar del Plata, Argentina. Mataifa ya Amerika yagawanyika.

6 Novemba 2005
https://p.dw.com/p/CELK

Mkutano wa mataifa ya Amerika umemalizika bila kupatikana makubaliano ya kusukuma mbele mapendekezo yanayoungwa mkono na Marekani yanayotaka kuifanya Amerika ya kaskazini na kusini kuwa eneo moja la biashara huria.

Maafisa wa Marekani wamesema mataifa 29 kati ya 34 yaliyowakilishwa katika mazungumzo hayo katika mji wa kitalii wa Mar del Plata nchini Argentina wanaunga mkono mpango huo wa kuunda kile kitakachojulikana kama eneo la biashara huria la bara la Amerika ama FTAA.

Lakini rais Hugo Chavez wa Venezuela ameongoza upinzani wa mapendekezo hayo.

Siku ya Ijumaa , aliwaambia waandamanaji wanaopinga mpango huo wa eneo huria la biashara katika maandamano yaliyomalizikia katika uwanja wa mpira kuwa anamipango ya kuuzika mpango huo.

Mkutano huo wa siku mbili uligubikwa na ghasia za maandamano ya kuipinga Marekani.