1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yazuka kati ya waasi na jeshi la Congo

18 Februari 2022

Mapambano makali yanaripotiwa kwa mara nyingine tangu mapema leo asubuhi kwenye eneo la Bibokoboko katika wilaya ya Fizi kati ya jeshi la Kongo FARDC na wanamgambo Mai-Mai Yakutumba

https://p.dw.com/p/47E2x
Demokratische Republik Kongo | Unruhen in Beni
Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Mapambano hayo kati ya jeshi la Kongo na Mai-Mai Yakutumba yanafanyika Bibokoboko ndani ya kijiji cha Majaga, eneo la Mutambala mashariki ya Kongo.

Kulingana na asasi za kiraia wilayani Fizi, mapigano yalianza tangu Jumanne baada ya shambulio la kundi hilo la wanamgambo wenye silaha dhidi ya vikosi vya jeshi la Kongo katika kijiji hicho ambapo kulikuwa kambi kubwa ya wakimbizi, wengi wao wakiwa wa kabila la Banyamulenge waliohama vijiji vyao muda mrefu kutokana na ukosefu wa usalama. Mawakili Kitandala Santos mwanasheria na msimamizi pia wa asasi za kiraia katika wilaya ya Fizi.

Soma pia: Wakaazi wa Ituri walalamikia ukosefu wa Usalama wa eneo hilo

Washuhuda mbalimbali wanaeleza kwamba kufuatia shambulizi hilo, wakimbizi wengi waliojihifadhi ndani ya kijiji hicho cha Bibokoboko wamekimbilia msituni, huku nyumba kadhaa zikiwa zimechomwa pia.

Demokratische Republik Kongo Süd-Kivu | Banyamulenge Community
Jamii ya Banyamulenge wilayani FiziPicha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Msemaji wa operesheni za kijeshi zinazoitwa Sukola yapili kusini mwa mkoa wa Kivu Kusini, Luteni Elongo Kyondwa Marc amebainisha kuwa jeshi limepambana vikali na wanamgambo hao tangu Jumanne, akihakikisha kwamba litaendelea kulinda usalama wa raia upande huo. ''Wakati wa shambulizi hilo, warugaruga hao wamewaua raia wanne siku ya Jumanne. Jeshi liliingilia kati kuzuia shambulizi hilo na limefaulu kuwaua wanamgambo kumi na nne. Jeshi la Kongo linawataka raia kuwa watulivu katika eneo hilo.''

Msemaji huyo wa jeshi amesema kwamba matokeo ya mashambulizi yanayofanyika wakati huu bado hayajulikani.

Kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, mbunge wa zamani wa kitaifa Enock Sebineza amelaani mashambulizi yanayofanyika kila siku na Mai-mai dhidi ya vijiji vya raia wa Banyamulenge na makundi ya kigeni yanayoungana nao, akitaka serikali ya Kongo kuwajibika zaidi.

Katika ripoti yake ya hivi karibuni, Ofisi ya uratibu wa misaada ya kiutu ya Umoja wa Mataifa OCHA imeonya kwamba hali ya usalama imekuwa mbaya tangu katikati ya mwezi Desemba mwaka jana, wakati mapigano yalipolazimisha zaidi ya watu elfu nane kuhamia maeneo jirani ya Mikenge, Mikalati, Kipupu, Tuwetuwe na Point Zero, wakiwa katika hali mbovu ya maisha.

Mitima Delachance, DW, Bukavu.