1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Mapigano ya Sudan yaingia siku ya sita na kuua watu 300

Sylvia Mwehozi
20 Aprili 2023

Milipuko na milio ya risasi imeendelea kuhanikiza mji mkuu wa Sudan, Khartoum wakati mapigano kati ya majeshi hasimu yakionyesha dalili za kutomalizika kuelekea sikukuu ya Eid baada ya kumalizika mfungo wa Ramadhan.

https://p.dw.com/p/4QLGn
Sudan Khartoum | Wakaazi wa Sudan wakikimbia mapigano
Wakaazi wa Sudan wakikimbia mapigano baina ya majeshi hasimuPicha: AFP

Watu takribani 300 wameuawa tangu kuzuka kwa mapiganosiku ya Jumamosi baina ya vikosi tiifu kwa kiongozi wa kijeshi Abdel Fattah al-Burhan na naibu wake Mohamed Hamdan Dagalo anayeongoza kikosi cha Rapid Support forces RSF. Mapigano makali yameendelea katika mji mkuu wa Khartoum ulio na wakaazi milioni tano wengi wao wakikwama majumbani mwao bila ya umeme, chakula na maji.

Mapigano hayo yameingia siku ya sita leo(20.04.2023)) baada ya makubaliano mengine ya kusitisha machafuko kuvunjika jana Jumatano, huku milio ya risasi ikisikika na moshi mzito mweusi kushuhudiwa karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Khartoum pamoja na makao makuu ya jeshi.

Sudan RSF Luteni Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo
Kiongozi wa jeshi la RSF Mohamed Hamdan Dagalo Picha: Umit Bektas/REUTERS

Rais wa Kenya William Ruto ambaye ni miongoni mwa wapatanishi waliopewa jukumu la kutafuta amani Sudan, ametoa rai ya kusitishwa mapigano, akionya kuwa yanaweza kudhoofisha kanda nzima. 

Soma pia: Tanzania yalaani mapigano yanayoendelea Sudan

Rais Ruto pia amezitaka pande zinazohasimiana kuruhusu misaada ya kibinadamu na kushirikiana na ujumbe wa kutoka jumuiya ya kikanda ya Afrika Mashariki, na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Pembe ya Afrika - IGAD. Aidha Ruto ameongeza kuwa hali nchini Sudan "inageuka kuwa kitisho kwa amani na usalama wa kikanda na kimataifa" na kuelezea hali ya kusikitisha kwamba wanadiplomasia wanalengwa katika mapigano hayo. Ruto ameongeza kwamba; 

"Pia tuna wasiwasi mkubwa kwamba wanachama wa jumuiya ya wanadiplomasia wanalengwa na raia kwa ujumla wamenaswa katika mapigano hayo. Mtindo wa ukiukaji utaratibu na kanuni zilizowekwa za sheria ya kimataifa ya binadamu, unajitokeza wazi na hali hii inageuka na kuwa tishio kwa amani na usalama wa kikanda na kimataifa."

Sudan | Mapigano mjini Khartoum
Wakaazi wakusanyika kununua mkate mjini KhartoumPicha: El-Tayeb Siddig/REUTERS

Kikosi cha RSF kilisema awali kwamba wanajeshi wake "wangeheshimu kikamilifu usitishaji mapigano" kuanzia saa 12 jioni siku ya jumatano kwa muda wa saa 24 kama litakavyofanya jeshi. Lakini mashuhuda wanadai kwamba milio ya risasi haikukoma mjini Khartoum katika muda uliotajwa na iliendelea hadi usiku ambapo makubaliano mengine ya kusitisha mapigano yamepuuzwa, dakika chache baada ya muda uliotakiwa kuanza kutumika.

Maafisa wa matibabu wameonya juu ya janga la kiafya hususan katika mji mkuu wa Khartoum, ambako hopsitali nyingi zimenaswa katika mapigano hayo. Nchi nyingi zimeanza kufanya mipango ya kuwahamisha maelfu ya raia wake wa kigeni kutoka Sudan lakini juhudi hizo zinatatizwa na mapigano yanayoendelea.