1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

RSF wakubali kusitisha mapigano kwa saa 24

Angela Mdungu
19 Aprili 2023

Wapiganaji wa kikosi maalumu cha wanamgambo wa RSF nchini Sudan wamekubali kuweka silaha chini kwa kipindi cha saa 24 kuanzia saa kumi na mbili kamili jioni leo Jumatano

https://p.dw.com/p/4QJCR
Sudan l Kämpfe im Sudan halten an l Rauch über Khartoum
Picha: Ahmed Satti/AA/picture alliance

Ni hatua iliyofikiwa baada ya wapiganaji hao kupambana na jeshi rasmi la serikali na kusababisha umwagaji damu kwa siku kadhaa wakigombea madaraka.

Taarifa iliyotolewa na wapiganaji wa kikosi cha RSF imeeleza kuwa wanathibitisha kuwa watakuwa waaminifu katika kusitisha mapigano na wanatumaini kuwa upande wa pili utaheshimu hatua hiyo kwa kufuata muda uliotangazwa. Haikuwa wazi ikiwa jeshi nalo lingetangaza kuheshimu usitishwaji wa mapigano.

Awali Jumanne, pande hizo mbili hasimu zilitangaza kukubali kuweka chini silaha lakini Shirika la habari la Reuters liliripoti kuzuka tena kwa mapigano usiku na  alfajiri ya leo mashariki mwa mji mkuu, Khartoum.:

Soma zaidiSudan: Kuna kauli zinazokinzana juu ya usitishaji mapigano

Katika hatua nyingine, kamisheni ya umoja wa ulaya kupitia msemaji wake Dana Spinant imesema kuwa mkuu wa ofisi ya masuala ya kiutu wa kamisheni ya Ulaya risasi nchini Sudan.

Kwa mujibu wa gazeti la The New York Times, afisa huyo wa juu wa Kamisheni ya ulaya aliyepigwa risasi ni  Wim Fransen, raia wa Ubelgiji na kwamba alikuwa akipatiwa matibabu kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata. 

Miili yaonekana mitaani

Nao raia wa Sudan waliokwama kwenye nyumba zao kwa siku kadhaa wameukimbia mji mkuu Kharthoum leo Jumatano ambapo mashuhuda wanasema miili ilionekana ikiwa imetapakaa mitaani kutokana na mapigano kati ya jeshi rasmi na wapiganaji wa kikosi cha RSF.

Wakati hayo yakiendelea, baadhi ya mataifa yameanza juhudi za kuwaondoa raia wake  Sudan. Serikali ya Japan imesema leo kuwa imeanza kujiandaa kuwaondoa raia wake nchini humo na inakuwa nchi ya kwanza kutangaza hadharani mipango hiyo.

Sudan General Abdel-Fattah Burhan
Mkuu wa Jeshi la Sudan Jenerali Abdel-Fattah BurhanPicha: Uncredited /ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Katika hatua nyingine serikali ya Ujerumani imeufuta mpango wake wa kuwaondoa raia wake nchini Sudan kwa wakati huu kutokana na hali ya usalama nchini humo. Uwanja wa ndege katika mji mkuu Khartoum umekuwa kitovu cha mapigano katika siku za hivi karibuni

Nao wawakilishi wa balozi mbalimbi nchini humo wametoa wito kwa pande mbili hasimu nchini humo kuweka silaha chini na kuheshimu wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ili kuwalinda raia, wanadiplomasia na wafanyakazi wa miisaada ya kiutu.