1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

Mapigano mapya yazuka kusini mwa Sudan

15 Desemba 2023

Mapigano kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF kwenye viunga vya mji wa Wad Madani yamepelekea familia za wakimbizi wa ndani kulazimika tena kukimbia vita hivyo ambavyo vimeingia mwezi wake wa tisa.

https://p.dw.com/p/4aEAk
Sudan | Kämpfe in Khartum
Raia wa Sudan wakielekea kwenye Hospitali Kuu ya mji wa Wad Madani: 25/05/2023Picha: AFP/Getty Images

Jeshi la Sudan limewazuia raia kuingia katika mji wa Wad Madani wakati linaendelea leo hii kukabiliana na mashambulizi ya wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF).

Mapigano hayo yameripotiwa takriban kilomita 180 kusini mwa mji mkuu Khartoum ambako awali lilikuwa kimbilio salama kwa raia wa Sudan vilipozuka vita kati ya wanajeshi na  wanamgambo wa RSF Aprili 15 mwaka huu.   

Mwandishi wa shirika la habari la AFP ameshuhudia ndege za kivita angani, moshi mweusi ukitoka eneo hilo ambako milipuko pia imesikika kutoka katika viunga vya kaskazini mwa mji huo. Wad Madani ni mji mkuu wa jimbo la Al Jazira, ambako kulingana na Umoja wa Mataifa, eneo hilo limekuwa kimbilio la watu nusu milioni waliokimbia makazi yao.    

Sudan Flüchtlinge auf einem Lastwagen
Raia wa Sudan wakiukimbia mji mkuu Khartoum uliokuwa ukikumbwa na vita (22.06.2023) kuelekea mji wa Wad Madani.Picha: AFP

Awali mji huo unaotegemea zaidi kilimo uliepuka kukumbwa na vita hivyo lakini  katika miezi ya hivi karibuni umeshuhudia wapiganaji wakivamia eneo hilo na kuwakusanya askari na kuweka vituo vya ukaguzi kwenye vijiji kati ya Khartoum na Wad Madani.

Kulingana na makadirio ya taasisi inayofuatilia matukio ya migogoro, vita kati ya mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan na makamu wake wa zamani, kamanda Mohamed Hamdan Daglo, vimegharimu maisha ya zaidi ya watu 12,190. Umoja wa Mataifa unakadiria pia kuwa watu zaidi ya milioni 5.4 wamekuwa wakimbizi wa ndani na karibu wengine milioni 1.5 wameikimbia kabisa nchi hiyo. 

Soma pia:  WFP: Sudan hatarini kukumbwa na baa kubwa la njaa

Hali iliyoshuhudiwa leo Ijumaa huko Wad Madani ilikumbushia hali ya kutisha ya siku za kwanza za vita huko Khartoum. Maduka na biashara zilifungwa kwa haraka huku watu wakiingia barabarani. Kwenye mitandao ya kijamii, baadhi walisambaza picha za watu wakiwa wamepakia mali zao huku wengine wakiulizia kuhusu njia salama ya kutoka katika mji huo wa Wad Madani.    

Shutuma za mateso kwa raia

Sudan | die Generäle Abdel Fattah Abdelrahman al-Burhan und Mohamed Hamdan Dagalo
Mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan akiwa na Mkuu wa kikosi cha RSF Mohamed Hamdan Daglo: 22.09.2021Picha: Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Wanamgambo wa RSF ambao hivi karibuni wameibuka na kasi ya utekaji wa miji mikubwa huko Sudan, wamekuwa wakituhumiwa kwa vitendo vya kinyama kama ubakaji, uporaji, mauaji na kuwaweka watu kizuizini kiholela.

Hata hivyo RSF imesisitiza leo katika taarifa yake na kuwahakikishia wale iliyowaita "raia wapendwa" huko Al Jazira na Wad Madani kwamba lengo la vikosi vyao ni kuwalinda raia na kuharibu ngome za jeshi.

Lakini pande zote mbili katika  mzozo huo wa Sudan  zimekuwa zikishutumiwa kwa uvamizi wa makombora katika maeneo ya makazi, pamoja na kuwalenga, kuwapora na kuwanyanyasa raia.

 

(Vyanzo: AFP,RTR)