Barack afanikiwa kutekeleza lengo lake.
25 Machi 2009Kiongozi wa chama cha Leba nchini Israel Ehud Barack amefanikiwa kutekeleza lengo lake. Chama chake kitaingia katika serikali ya mseto na chama cha kihafidhina -Likud,cha waziri mkuu mteule, Benjamin Netanyahu.
Chama cha Leba kimemsaidia kiongozi wa chama cha Likud kuingia madarakani.
Kiongozi wa chama cha Leba Ehud Barack alipata asilimia 58 ya kura zilizomuunga mkono.
Barack amefanikiwa kutekeleza shabaha yake baada ya mazungumzo ya usiku kucha na kiongozi wa chama cha Likud, Netanyahu.
Chama cha Leba ambacho kwa miaka mingi kilikuwa chama cha mstari wa mbele,mwasisi wa nchi na kiongozi wa serikali ya kwanza ya Israel kilimaliza katika nafasi ya nne katika uchaguzi mkuu uliopita.
Kiliambulia viti 13 katika bunge lenye viti 120.
Kujiunga na serikali ya mseto hakutazuia kuanguka kwa chama hicho bali hatua hiyo itaharakisha kuanguka huko.
Kwa wanachama wengi wa chama hicho,Barack amechukua hatua hiyo ili kutekeleza maslahi yake binafsi.
Ni wazi kwamba bwana Barack hatakiri hayo, kwani akifanya hivyo atakuwa anajisuta mwenyewe . Wakati wa uchaguzi alizungumzia juu ya kuingia katika upinzani.Lakini sasa amegeuza kauli.
Amesema kuwa hamwogopi Netanyahu na kwamba ataleta urari katika mizani ya serikali dhidi ya sera zote za mwelekeo mkali wa kulia.
Amehoji kuwa kama mshiriki katika serikali ya mseto ataweza kufikia mengi zaidi kuliko kuwa katika upinzani na viti 13 tu.
Yumkini inaweza kuwa hivyo lakini swali ni, Ehud Barack anaweza kutimiza na kupata nini katika serikali kama hiyo.? Yaani serikali itakayoongozwa na waziri mkuu aliesema katika kampeni za uchaguzi kwamba hana haja kubwa ya kuanzisha tena mazungumzo ya kuleta amani.
Atapata nini katika serikali ambapo waziri wa mambo ya nje anatazamiwa kuwa mtu anaeitwa Avigdor Liebermann mwanasiasa mwenye itikadi kali za mrengo wa kulia-mwanasiasa alietishia kuliteketeza bwawa la Asuan nchini Misri.Mwanasiasa huyo anawaona waisraeli wenye nasaba ya kiarabu kuwa maadui wa nchi na ambae angetaka kuona Iran ikishambuliwa leo badala ya kesho.
Matatizo na migongano imeshajenga mizizi ndani na nje ya Israel.
Tayari pana sauti kutoka Umoja wa Ulaya zinazosema kuwa haitawezekana kushirikiana na serikali hiyo ya mrengo mkali wa kulia.Pana wasi wasi nchini Marekani vilevile.Serikali hiyo pia itaimarisha mtazamo wa waarabu ambao wakati wote wamekuwa wanasema kuwa Israel haitaki amani.
Kwa kuingia katika serikali ya mseto na chama cha Likud Ehud Barack amerudisha nyuma matumaini ya amani.