1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Mchakato wa Brexit Je safari hii Bunge litauridhia?

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
18 Oktoba 2019

Umoja wa Ulaya umefikia mkataba mwingine na serikali ya Uingereza. Hata hivyo haijulikani iwapo bunge la nchi hiyo litaupitisha mkataba huo. .

https://p.dw.com/p/3RWiY
Belgien Brüssel EU Gipfel | Boris Johnson
Picha: Getty Images/AFP/K. Tribouillard

Mambo bado hayajafikia tamati. Umoja wa Ulaya umefikia mkataba na serikali ya Uingereza kwa mara nyingine. Wakati pana hisia za bashasha nchini Uingereza, kwenye Umoja wa Ulaya watu wanakumbuka kwamba walishawahi kuwapo mahala hapo hapo pamoja na Theresa May Waziri Mkuu wa zamani.

Na kama ilivyokuwa hapo awali, safari hii pia uwezekano wa mkataba huo mwingine kupitishwa na bunge ni finyu. Wabunge wengi wana mashaka, kwa sababu wanaona bora kubakia kwenye Umoja wa Ulaya. Wengine wana wasiwasi juu ya mipango ya baadae ya Waziri Mkuu wa sasa Boris Johnson kuhusu Uingereza itakayosimama mbali zaidi na Umoja wa Ulaya kuliko ambavyo May alivyopendekeza. Safari hii pia itakuwa vigumu kupatikana idadi ya wabunge wa kuunga mkono mkataba huo mwingine.

Kushoto: Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Ireland leo Varadkar. Kulia Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson
Kushoto: Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Ireland leo Varadkar. Kulia Waziri Mkuu wa Uingereza Boris JohnsonPicha: Reuters/P. Noble

Sababu pekee ya kuwapo uwezekano wa aina yoyote ni kwamba Waziri Mkuu wa Ireland, Leo Varadkar alimpa Johson pendekezo la ukarabati juu ya kulitatua suala la Ireland. Johnson anatambua kwamba katika muktadha wa mkwamo uliopo nchini mwake, njia pekee iliyobakia kwake ni kusonga mbele na mkataba juu ya nchi yake kujiondoa Umoja wa Ulaya. Na kwa hivyo amejibadilisha kama kinyonga na kujifanya ameyasahau aliyoyasema jana tu: amesahau juu ya uwepo wa Ireland Kaskazini ndani ya Uingereza jambo ambalo May alilitetea kwa ukali wote.

Mkataba uliofikiwa unafanana sana na ule wa awali uliolenga shabaha ya kuepuka kuwapo kwa mpaka wa kufunga milango baina ya Ireland Kaskazini na Jamhuri ya Ireland. Umoja wa Ulaya pia ulipendekeza suluhisho hilo katika mkataba wa mwanzo. Umoja huo umekubali kwamba Ireland Kaskazini inaweza kujiondoa rasmi kwenye umoja wa forodha lakini italazimika kufuata sheria za Umoja wa Ulaya ili kuidumisha hali ilivyo sasa, kati ya nchi mbili za Ireland. Hata hivyo masuala muhimu hayahusu uchumi na biashara tu. La msingi zaidi ni masuala ya utambulisho wa watu na maisha yao ya kila siku.

Umoja wa Ulaya na Jamhuri ya Ireland zinaweza kuwa hazina taabu na mwafaka uliofikiwa. Umoja wa Ulaya umehakikisha kwamba umeweka muhuri wa kuwezesha kutekelezwa kwa haki zake. Mkataba uliofikiwa ni mzuri sana kwa jumuiya hiyo. Katika upande mwingine mkataba huo utamuwezesha Johnson kujigamba kwamba ameiondoa  Uingereza yote kutoka Umoja wa Ulaya na kwa hivyo nchi hiyo sasa itaudhibiti mustakabali wake juu ya kila kitu. Hiyo ni sehemu ya propaganda ingawa hayo si ya kweli.

Kiongozi wa chama cha DUP Arlene Foster
Kiongozi wa chama cha DUP Arlene FosterPicha: Reuters/H. Nichollls

Mkataba sasa upo mezani lakini hakuna uhakika iwapo utapitishwa na wabunge hapo kesho. Ikiwa chama cha DUP cha Ireland Kaskazini kitaupinga mkataba huo kwa sababu ya kuifanya nchi hiyo ipate hasara kubwa zaidi kuliko faida, basi Johnson atapoteza mshirika thabiti wa Brexit. Na hakuna uhakika iwapo wabunge aliowafukuza kutoka kwenye chama kijeuri, watakuwa tayari kusimama pamoja naye bungeni.

Ni wazi kwamba kimsingi chama cha upinzani cha Labour kinaupinga mkataba huo mwingine, ukiondoa wabunge wachache wa chama hicho. Labda Waziri Mkuu Johnson atafanya muujiza hapo kesho, la sivyo suala la Brexit litarudi pale pale lilipoanzia jambo ambalo Umoja wa Ulaya unataka limalizike haraka!

Na inapasa kutambua kwamba hata ikiwa Uingereza itajiondoa Umoja wa Ulaya vuta nikuvute itaendelea. Mazungumzo juu ya kipindi cha mpito yatachukua muda wa mwaka mmoja. Na ikiwa Uingereza haitaomba kuongezewa muda wa Brexit, nchi hiyo itajitosa kizani. Kila nyanja ya uhusiano wa hapo baadae itapaswa kujadiliwa upya na Umoja wa Ulaya. Kwa ufupi Waingereza wanauziwa sanduku la mkakasi kwani mazungumzo juu ya mambo ya biashara yatakuwa ya kukaziana macho. Umoja wa Ulaya umeonyesha kuwa huataki mzaha.

Chanzo/ https://p.dw.com/p/3RTgh