Mamlaka Kenya zakanusha kuwateka wakosoaji wa serikali
27 Desemba 2024Haya yanajiri baada ya vijana 4 kutoweka siku chache zilizopita katika mazingira ya kutatanisha. Wakati huohuo, kulingana na tume ya kutetea haki za binadamu, KNCHR, visa 13 vya utekaji vimeripotiwa katika miezi mitatu pekee iliyopita.
Soma pia: Polisi Kenya yakanusha kuhusika na utekaji wa wakosoaji
Kwa mujibu wa taarifa ya idara ya upelelezi nchini Kenya,DCI iliyosambazwa kwa vyumba vya habari saa chache zilizopita,taasisi hiyo kamwe haijahusika na utekaji wa wanaharakati kama ilivyodaiwa.Taarifa hiyo ilizuka baada ya Seneta wa kaunti ya Busia,Okiya Omtatah kudai kuwa mwanaharakati Kibet Bull almaarufu Yoko, alitekwa na watu waliotumia gari jeupe aina ya Subaru Forester lililokuwa na nambari bandia ya usajili. Kisa hicho kilitokea baada ya mkutano kati ya Seneta wa Busia Okiya Omtatah na Kibet Bull katika eneo la Upper Hill jijini Nairobi.
Soma pia: Wakenya waliotoweka waachiwa huku mashirika ya haki yakivilaumu vikosi vya usalama
Seneta Omtatah yuko mbioni kuwasilisha mswada wa kushinikiza uchunguzi wa dharura kufanyika mintarafu visa vya utekaji vinavyoshuhudiwa. Ucunguzi huo unadhamiria kuhusisha visa vilivyotokea tangu mwezi wa Juni mwaka huu kufuatia maandamano ya kupinga mswada wa fedha uliokuwa na utata.
Kwa upande wake, tume ya kutetea haki za binadamu nchini Kenya, KNCHR, imeiweka idadi ya waliotekwa na kutoweka tangu wakati huo kuwa 82 ilielezea taarifa ya mwenyekiti wake Roseline Odede. KNCHR imebaini kuwa katika muda wa miezi mitatu iliyopita pekee watu 13 wametoweka katika mazingira ya kutatanisha. Matukio hayo yamewawia viongozi wa kidini kukashifu vitendo hivyo kama anavyoelezea mwenyekiti wa baraza la maaskofu wa kanisa katoliki nchini Kenya, KCCB, Askofu Martin Kivuva wa dayosisi ya Mombasa.
Kwa upande wake idara ya mahakama ya Kenya imetahadharisha kuwa sheria sharti zifuatwe na haki kudumishwa hasa na idara na taasisi za usalama. Kwenye taarifa yake iliyochapishwa saa chache zilizopita, idara ya mahakama inashikilia kuwa utekaji na kutoweka hakuna nafasi kwenye mipaka ya Kenya kikatiba. Wakenya wana mtazamo upi kuhusu utekaji unaoripotiwa? Nuru Okanga ni mkereketwa kutokea mtaa wa Kayole na anashikilia kuwa hali inatisha.
Tangu mwanzoni mwa wiki,wanaharakati kadhaa waliripotiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha nao ni Billy Mwangi, Peter Muteti, Bernard Kavuli, na Naomi kutokea kaunti za Embu, Nairobi na Kajiado.Wanne hao wamekuwa wakitoa maoni yao mtandaoni.