Polisi Kenya yakanusha kuhusika na utekaji wa wakosoaji
26 Desemba 2024Vikosi vya usalama Kenya vimetuhumiwa na mashirika kadhaa ya haki za binaadamu kwa kuwateka na kuwaweka kizuizini kinyume cha sheria watu kadhaa tangu maandamano makubwa ya kuipinga serikali ya Juni na Julai mwaka huu.
Soma pia: Wakenya waliotoweka waachiwa huku mashirika ya haki yakivilaumu vikosi vya usalama
Mkuu wa polisi nchini Kenya Douglas Kanja amesema katika taarifa kuwa jeshi la polisi limeshtushwa na madai yanayoendelea kwamba maafisa wa polisi wanahusika na utekaji wa watu nchini humo.
Matukio ya karibuni ya utekaji kwa mara nyingine yaliwalenga watumiaji wa mitandao ya kijamii walioikosoa serikali ya Rais William Ruto. Vijana hao wa umri usiozidi miaka 23 -- Peter Muteti, Billy Mwangi na Bernard Kavuli-- wote walitoweka mwishoni mwa wiki ililiyopita. Mtu wa nne, ambaye hajatajawa, pia aliropotiwa kuchukuliwa katika siku za karibuni. Wakati polisi ikikanusha kuhusika kwake, haijasema kama imepiga hatua katika kuwatambua wanaohusika na utekaji huo. Tume ya Kitaifa ya Haki za Binaadamu ilisema mapema mwezi huu kuwa karibu watu 74 walitekwa tangu maandamano ya kuipinga serikali, huku 26 wakiwa bado hawajulikani waliko.