1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makundi ya waasi yasababisha mauaji Mashariki mwa Congo

20 Machi 2023

Watu zaidi ya 20 wameuwawa katika matukio mawili tofauti ya mashambulizi Mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, ambako bado kunashuhudiwa mapigano kati ya wanajeshi wa serikali na waasi wa M23.

https://p.dw.com/p/4OvTm
DR Kongo | Unruhen in Nord-Kivu
Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Katika jimbo la Kivu Kaskazini mapigano yaliripotiwa siku ya Jumamosi kati ya wanajeshi wa serikalli na waasi wa M23  siku kadhaa baada ya utulivu kiasi kushuhudiwa katika eneo hilo. Kwa sasa Kikosi cha wanajeshi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC kimepelekwa huko ili kudhibiti hali.

Kundi la M23 linaotokea kabila la watutsi limeendelea kuyateka miji kadhaa nchini Congo na kusonga mbele kutaka kuukamata pia mji wa kimkakati wa Goma, hali iliyosababisha Jumuiya ya EAC mwezi Novemba mwaka jana kushinikiza vikosi vyake kupelekwa huko.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wawasili DRC

Katika taarifa yake jeshi la DRC limesema wapiganaji wa M23 waliyashambulia maeneo yao sita hatua inayokiuka makubaliano ya kusitisha mapigano yaliopaswa kuanza kutekelezwa tarehe 7 mwezi Machi.

DRC na serikali za Mataifa ya Magharibi zinadai kwamba waasi wa M23 wanaungwa mkono na Rwanda na kwamba wana nia ya kuchukua rasilimali zilizopo eneo la mpakani madai ambayo Rwanda inaendelea kukanusha.

Mashambulizi mengine yaripotiwa mjini Mahagi na Nguli

DR Kongo | Unruhen in Nord-Kivu
Baadhi ya wanamgambo wa FRPI, Congo wanaodai kuwalinda watu wa jamii ya Walendu katika Jimbo la Ituri Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Kwengineko Arnold Lokwa chifu katika jimbo la Ituri, amesema kundi la wanamgambo la CODECO linalodai kuwalinda jamii ya walendu kutoka kwa kundi jingine la wanamgambo la Hema, linadaiwa kuvilenga vijiji vitano katika mji wa Mahagi jimboni humo siku ya Jumamosi.

Lokwa ameongeza kuwa hadi sasa wamehesabu miili ya watu 15 wengi wakiwa wanawake, watoto na wazee. Watu wengine 9 waliripotiwa kuuwawa pia katika kijiji kingine jirani cha Nguli.

Chifu wa eneo hilo Kambale Kamboso amesema Mauaji hayo yanadaiwa kufanywa na kundi la wanamgambo la Allied Democratic Forces (ADF) linalofungamanishwa na kundi la dola la kiislamu IS lililokiri kuhusika na shambulio hilo, kupitia shirika la habari la Amaq lenye mafungamano nalo.

ADF wauwa wanavijiji 17 DRC

Kambale Kamboso aliliambia shirika la AFP kwamba watoto wawili hawajulikani waliko baada ya shambulio hilo lililotekelezwa kwa kutumia visu na mapanga.

Kundi hilo la waasi la ADF linaloaminika kutokea nchini Uganda, liliingia nchini Congo miaka ya 1990 na tangu wakati huo limekuwa likidaiwa kuhusika na mauaji ya maelfu ya watu nchini humo. 

Chanzo: afp/reuters