1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makumi ya wabunge Kenya wakutwa na kirusi cha Omicron

Shisia Wasilwa23 Desemba 2021

Makumi ya wabunge na wafanyakazi wa idara ya bunge nchini Kenya wameambukizwa na covid-19,baada ya kurejea kutoka nchi jirani ya Tanzania walipokuwa kwenye michezo.

https://p.dw.com/p/44kIg
Symbolbild Impfpass Coronavirus Impfung Spritze
Picha: Fleig/Eibner-Pressefoto/picture alliance

Kwa mujibu wa duru hizo, wafanyakazi 41 walioandamana na wabunge hao katika michezo ya wabunge iliyoandaliwa mjini Arusha, wamepatikana na virusi vya Omicron. Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Karani wa Bunge la Taifa, Michael Sialai, amekiri kuwa afisi yake inafahamu kuwa kuna usambaaji wa virusi hivyo baada ya wafanyakazi kupimwa.

Kwenye taarifa hiyo, Sialai ameongeza kusema idadi kubwa ya wabunge na wafanyakazi wamepatikana na virusi hivyo na wametakiwa kujitenga kwa mujibu wa mwongozo wa wizara ya afya.

Sialai amehakikishia umma kuwa, tahadhari zote zimechukuliwa kwa kuzingatia utaratibu wa kukabiliana na virusi hivyo katika majengo ya bunge. Haijabainika idadi ya kamili ya watu waliokuwamo wkenye ujumbe kutoka Kenya waliokwenda kwenye michezo ya Arusha, Tanzania, kati ya tarehe 4 hadi 17 mwezi huu.

Soma pia:Watu 12 wauawa Marsabit

''Tunahitaji kuendelea kuchanjwa''

Coronavirus Afrika | Kenia Impfungen
Picha: SIMON MAINA/AFP/Getty Images

Hayo yanajiri huku viwango vya kusambaa kwa virusi hivyo vikiongezeka mara tano zaidi msimu huu wa Krismasi. Daktari Patrick Amoth ni mkurugenzi wa Wizara ya Afya.

"Tunatarajia kuwa hatutapitisha asilimia 30 ya maambukizo na kwamba tutasalia pale pale. Itatulazimisha kupunguza, ili kufikia hayo tunahitaji kuendelea kuchanjwa.”

Wabunge wa mataifa ya Tanzania, Burundi, Uganda, Kenya na wenzao wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walikuwa na mashindano katika nyanja mbalimbali. Maambukizi sawa na hayo yameripotiwa katika taifa jirani la Uganda ambapo wabunge 50 wamepatikana na virusi hivyo vya Omicron.

Soma pia:Kenya: Sharti wageni wathibitishe wamepata chanjo ya COVID

Ongezeko la maambukizi ya virusi vya Corona nchini Kenya

Coronavirus Afrika | Kenia Impfungen
Picha: SIMON MAINA/AFP/Getty Images

Viwango vya maambukizo vimekuwa asilimia 6 tangu sherehe za Jamhuri zilizoandaliwa tarehe 12, lakini vimeongezeka na kufikia 30 jana jioni. Hali hiyo imeilazimisha serikali kutangaza masharti makali. Katibu katika wizara ya afya Mercy Mwangangi ametangaza kuwa Wakenya watahitajika kuonesha vyeti vyao vya chanjo ya COVID-19 ili kupokea huduma za msingi.

"Utahitaji kuonesha cheti cha chanjo katika afisi zote za serikali. Masharti hayo pia yatazingatiwa kwenye hafla zote zitakazofanywa.”

Cheti hicho pia kitahitajika katika maeneo ya umma kama vile makumbusho, migawahani, benki, hidafhi za mbuga na afisi za serikali.

Hata hivyo. tamko la wizara ya afya linakiuka agizo la Mahakama Kuu nchini Kenya iliyosimamisha agizo hilo linalowaamuru Wakenya kuchanjwa dhidi ya ugojwa wa Covid-19 kabla ya kupokea huduma za msingi.