1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 12 wauawa Marsabit

20 Desemba 2021

Watu kumi na wawili wamethibitishwa kuuawa katika hujuma ya wizi wa mifugo katika jimbo la Marsabit nchini kenya.

https://p.dw.com/p/44YzW
BG Kenia Turkana Kriger
Picha: Reuters/G. Tomasevic

Watu hao walivamia vijiji vya Kubi Kallo na Jaldesa katika eneo bunge la Saku siku ya jumamosi.

Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi Jimbo la Marsabit Robinson Mboloi, magenge ya wahalifu waliokuwa na bunduki, walivamia vijiji hivyo na kuwapiga watu risasi kabla ya kupora mifugo zaidi ya elfu moja ambayo polisi walifanikiwa kuirudisha.

Kamanda huyo wa polisi pia amesema uchunguzi unaendelea kuhusu tukio hilo huku akiwataka wananchi kutoa taarifa zitakazosaidia idara ya polisi kuwakamata wahusika.

Gavana wa jimbo la Marsabit Muhamud Ali amesikitishwa na hatua ya kuzorota hali ya usalama katika jimbo hilo na amezitaka asasi za kiusalama kuongeza juhudi kuwakamata wahalifu hao.

Mauaji hayo yanajiri wakati mkutano wa amani wenye lengo la kusitisha mapigano ukitarajiwa kuanza leo jimboni humo

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW