1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Makomando wa Afghanistan wapambana na Taliban Herat

Josephat Charo
2 Agosti 2021

Maafisa wa vikosi vya Afghanistan wamekabiliana na wapiganaji wa Taliban kwenye mapambano makali ya barabarani na kuyashambulia kwa mabomu maeneo yao wakati wanamgambo hao walipoishambulia miji mikubwa.

https://p.dw.com/p/3yPbu
Afghanistan Unruhe in der Provinz Herat
Picha: Shoaib Tanha/DW

Mamia ya makomando wa Afghanistan wamepelekwa katika mji wa magharibi wa Herat huku vikosi vya serikali vikijizatiti kupambana na wapiganaji wa Taliban katika miji kadhaa mikubwa wakati wanamgambo hao wakiimarisha operesheni yao ya nchi nzima kabla kuondoka kabisa kwa wanajeshi wa nchi za kigeni kufikia Agosti 31. Makomando hao wamepelekwa mji wa Herathuku maafisa katika mji wa kusini wa Lashkar Gah wakiitisha wanajeshi zaidi kudhibiti mashambulizi ya Taliban.

Mwanajeshi mmoja wa Afghanistan kwa jina Mohammed amesema ni mwanachma wa vikosi maalumu vya nchi hiyo na wamekwenda Herat kuwasaidia watu. Mwanajeshi huyo pia amesema wapo katika uwanja wa vita lakini kuna msaada kutokea angani na maafisa wa kutosha wa vikosi vya usalama na wako huko kusafisha.

Mwanajeshi mwingine kwa jina Naser Alizai naye alisema, "Idadi ya wapiganaji wa Taliban na sare zao haifahamiki. Kwa kutumia nyumba za makazi na kwa kuvaa nguo za kawaida za kiraia wanapita uwanja wa vita na kuingia maeneo na wanapokabiliwa na upinzani, wanaondoka. Taliban sio wakali sana, wanapigana wakiwa wametawanyika. Wanawafanya watu wawe na wasiwasi na kushusha morali wao."

Taulah Afghan, mkuu wa mkoa wa Helmand ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kuwa mapigano yanaendelea katika mji wa Lashkar Gah na wameomba msaada maafisa wa vikosi maalumu wapelekwe huko.

Hali ni ngumu katika maeneo ya mapambano

Halim Karimi, Mkazi wa mji wa Lashkar Gah, wenye idadi ya wakati 200,000, amesema mji huo uko katika hali mbaya mno na hafahamu kitakachotokea. Karimi aidha amesema Taliban hawatakuwa na huruma nao na wanajeshi wa serikali hawataacha kuwashambulia kwa mabomu.

Afghanistan | Konflikt in Laschkar Gah | Afghanische Sicherheitskräfte
Hali si shwari Lashkar GahPicha: Sifatullah Zahidi/AFP

Nazar Mohammed, ni mkulima katika wilaya ya Injil. Alisema, 2Ni wiki moja tangu mapigano yalipoanza Herat. Watu wameathiriwa, kilimo kimeathiriwa, matunda ambayo watu walitaka kuyaleta sokoni kuyauza yameshaoza. Hali ya usalama ni ya kutia wasiwasi. Kila kitu kimekuwa ghali zaidi na watu wana wasiwasi sana."

Mbali kabisa upande wa magharibi  katika mji wa Herat mapigano yaliendelea katika viunga vya mji huo usiku kucha huku mashambulizi ya kutokea angani yakiyalenga maeneo ya Taliban, kufuatia siku moja ya makabiliano makali kati ya wanapiganaji hao na vikosi vya usalama vya Afghanistan wakisaidiwa na wapiganaji wa makundi ya waasi wa eneo hilo. Msemaji wa gavana wa Herat, Jailani Farhad, amesema wanamgambo takriban 100 wameuwawa katika mashambulizi hayo.

Wakati mapigano yalipokuwa yakiendelea rais wa fghanistan Ashraf Ghanikwa mara nyingine tena aliwakosoa Taliban kwa kushindwa kutumia nguvu yao kutafuta muafaka wa amani. Akizungumza kwenye kikao cha baraza la mawaziri Ghani amesema wanataka amani lakini Taliban wanataka serikali isalimu amri.

Tume ya amani ya Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan UNAMA pia imewakosoa Taliban ikiwataka wapiganaji hao watoe majibu kuhusu shambulizi la roketi dhidi ya afisi yake huko Herat Ijumaa iliyopita lililomuua mlinzi mmoja raia wa Afghanistan. Katika taarifa yake kwenye mtandao wa kijamii wa twitter UNAMA ilidokeza pia kulitokea matukio ya machafuko katika kambi moja ya jeshi huko Herat Jumamosi iliyopita, bila kutoa maelezo zaidi.

(afp)