1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Afghanistan waliofanya kazi na Marekani wahamishwa

30 Julai 2021

Kundi la kwanza la raia wa Afghanistan waliofanya na vikosi vya jeshi la Marekani limewasili Washington kuanza maisha mapya baada ya Marekani kuamua kuwapatia hifadhi kukwepa hujuma za wanamgambo wa Taliban.

https://p.dw.com/p/3yJi6
Symbolbild I US Armee in Afghanistan
Vikosi vya Marekani vilitegemea sana msaada wa raia wa Afghanistan katika kutekeleza majukumu yao.Picha: John Moore/Getty Images

Ndege iliyowabeba raia 221 wa Afghanistan ilitua Alfajiri ya leo mjini Washington ikijumuisha watoto zaidi ya 70 ambao wao na familia zao wataanza maisha mapya  nchini Marekani chini mpango maalum wa kutoa visa kwa Waafghani waliofanya kazi na vikosi vya Marekani.

Makundi mengine kama hayo yanatarajiwa kuwasili nchini Marekani katika wiki chache zinazokuja yakijumuisha watu waliofanya kazi ya ukalimani na shughuli nyingine kuvisaidia vikosi vya Marekani kutimiza jukumu lake nchini Afghanistan.

Chini mpango huo wa visa maalum zaidi ya Waafghani 2,500 pamoja na familia zao huenda watahamia nchini Marekani na kuanza maisha mapya.

Mpango huo wa visa maalum uliidhinishwa na bunge la Marekani mwaka 2006 ili kuwapatia hifadhi raia wa Iraq na Afghanistan ambao wamehatarisha maisha yao kwa kufanya kazi na serikali ya Marekani.

Maelfu wengine kunufaika na mpango wa visa maalum

Afghanistan, Kabul | Amtsübergabe von US-General Scott Miller an US-General Frank McKenzie
Wakati vikosi vya Marekani vikiondoka Afghanistan wasiwasi ni mkubwa kuhusu usalama wa raia wa nchi hiyo waliofanya kazi na vikosi vya kigeniPicha: Ahmad Seir/AP/picture alliance

Operesheni ya kuwahamisha raia hao inafanyika katika wakati vikosi vya Marekani vinakamilisha kujiondoa kikamilifu kwenye vita nchini Afghanistan baada ya karibu miongo miwili.

Kwa jumla Marekani na  washirika wake wanalenga kuwapatia hifadhi kiasi raia 50,000 wa Afghanistan katika juhudi za kuwalinda dhidi ya uwezekano wa kulengwa na kundi la wanamgambo wa Taliban ambalo liliondolewa madarakani wakati vikosi vya kigeni vilipoingia  nchini Afghanistan mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Kuongezeka kwa mashambulizi ya Taliban katika siku za hivi karibuni kumesababisha matatizo makubwa kwa Waafghani ambao bado hawajapatiwa majibu ya maombi ya kwenda kuishi Marekani.

Kuna ripoti kwamba wapiganaji wa kundi hilo wanawalenga wale waliofanya kazi na vikosi vya kigeni kwa lengo la kulipa kisasi.

Mapambano kati ya jeshi na kundi la Taliban yanaendelea 

Taliban-Offensive in Afghanistan | Qala-i- Naw
Picha: AFP/Getty Images

Wakati hayo yakijiri vikosi vya jeshi la Afghanistan vimesema jana kwamba vimezuia shambulizi la kundi la Taliban kwenye mji muhimu wa mashariki wa Herat, wakati kundi hilo la wanamgambo likizidisha operesheni yake ya kuyakamata maeneo makubwa nchini humo.

"Wanakuja wakiwa wamevaa kandambili na wanapigana dhidi yetu wakiwa na risasi moja lakini sisi tuna vifaa madhubuti ikiwemo vifaru na tutapambana nao" amesema mwanajeshi mmoja wa Afghanistan alipozungumza na shirika la habari la AFP.

Imeelezwa kuwa wanajeshi wa Afghanistan na wapiganaji wa mbabe wa kivita anayelipinga kundi la Taliban Ismail Khan, wamepelekwa kwenye mji huo wa wakaazi 60,000.

Hata hivyo jeshi la Afghanistan limesema mapigano ya kuwania mji wa huo Herat bado yanaendelea lakini linajizuia kusonga mbele ili kuepusha maafa zaidi kwa raia.