1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali Tanzania kuyafungulia magazeti yaliofungiwa

Hawa Bihoga20 Mei 2021

Serikali ya Tanzania imesema ipo kwenye majadiliano kuangalia utaratibu ambao utatumika kuyafungulia magazeti yaliofungiwa na sheria zinazotajwa na wadau wa habari kuwa zinaminya uhuru wa habari.

https://p.dw.com/p/3tgWh
Kassim Majaliwa, Premierminister von Tansania
Picha: Büro des Premierministers von Tansania

Hayo yamewekwa wazi na waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa alipofungua mkutano mkuu wa mwaka wa Jukwaa la Wahariri, ambao mbali na mambo mengine walimueleza juu ya changamoto ya sheria kandamizi ambazo zinaminyauhuru wa habari.

Majaliwa amesema kati ya magazeti manne yaliyofungiwa kutokana na sheria zinazotajwa na wadau kuwa ni kandamizi, wapo katika hatua ya kuridhisha ili kuyaruhusu yaendelee na kazi, kwani huo ni muelekeo wa rais wa sasa aliyeko madarakani Samia Suluhu Hassan kuhakikisha uhuru wa habari unatamalaki.

Soma pia: Maoni: Hali ngumu kwa vyombo vya habari Tanzania

Tanzania ina redio zaidi ya 150 na runinga zipatazo 45 kadhalika magazeti yaliyosajiliwa zaidi ya 250, na vyombo hivi vinavyotazamwa kama daraja baina ya mamlaka na umma vilikumbwa na hofu kwa takriban miaka mitano kutokana na sheria kandamizi.

Tansania Medienfreiheit verbotene Zeitung Mawio
Gazeti la Mawio ni mmoja kati ya manne yaliofungiwa wakati wa utawala wa awamu ya tano.Picha: Zuberi Mussa

Sheria hizo ikiwemo ile ya takwimu, sheria ya huduma za habari zilidaiwa na wadau kutumiwa kama fimbo na mamlaka kuvifungia vyombo vya habari na wakati mwingine vyombo hivyo viliamua kujiadhibu kwa kuuza uhuru wake ili kuepukana na rungu la mamlaka.

Marekebisho ya sheria yaja

Waziri Mkuu Majaliwa amesema tayari serikali imeshatoa maelekezo kuhusiana na marekebisho ya Sheria na kuwataka wadau hao wa habari kutumia kipindi hiki kuwasilisha mapendekezo yao ili sheria zinazolalamikiwa ziangaliwe upya na Bunge.

Soma pia: Tanzania yakanusha kukandamiza uhuru wa habari

Pamoja na hayo Jukwaa la Wahariri Tanzania TEF limeiomba serikali kurejesha utaratibu wa zamani wa usajili wa kudumu wa magazeti kuliko hivi sasa wanapopatiwa usajili wa muda ambao unatumiwa vibaya kuminya uhuru wa habari.

Endapo Tanzania itaziangalia upya sheria hizo itakuwa inatekeleza hukumu ya Mahakama ya Afrika Mashariki ambayo iliiamuru kupitiwa upya sheria zote ambazo zinalalamikiwa na wadau kuhusiana na uhuru wa vyombo vya habari kwani zinakwenda kinyume na itifaki ya Jumuiya Afrika Mashariki iliyowasilishwa na Asasi za Kiraia.