1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Majadiliano magumu juu ya makubaliano ya biashara ya mbao za nchi za joto

Joachim Schubert-Ankenbauer / Maja Dreyer18 Januari 2006

Biashara ya mbao za nchi za joto jingi inafika kiasi cha dola 10 za Kimarekani duniani kote. Hivyo katika nchi kadhaa zinazoendelea biashara ya mbao ni sehemu muhimu ya uchumi. Upande mbaya wa biashara hiyo lakini ni kwamba inaathiri sana misitu ya asili katika nchi hizi.

https://p.dw.com/p/CHnx
Msitu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo unaoathiriwa na biashara ya mbao
Msitu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo unaoathiriwa na biashara ya mbaoPicha: dpa
Ili kulinda mazingira na wakati huo huo kuhakikisha nchi zisipoteze biashara hiyo, shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya biashara na maendeleo UNCTAD linajadili juu ya makubaliano mapya ya biashara ya mbao. Mkataba wa zamani unamalizika mwisho wa mwaka huu.

Makubaliano ya mbao ni moja kati ya makubaliano mengi ya mali ghafi yaliyopitishwa na shirika la UNCTAD, kama kwa mfano kuhusu biashara ya kakao, mafuta ya zeituni au pamba. Kwa hivyo ni mali ghafi ambazo zinauzwa na nchi nyingi zinazoendelea. Makubaliano haya yanatarajiwa kuhakikisha kwamba nchi hizi zitumie vizuri mali ghafi zao na hivyo kuendeleza uchumi wao. Pamoja na hayo makubaliano ya UNCTAD zinahitajika kuliweka soko wazi ili wauzaji na wanunuzi wana uhuru wa kukubali kuhusu bei, kiasi na kadhalika.

Makubaliano ya biashara ya mbao yana umuhimu mwingine, kama Carlos Paranhos anavyoeleza. Huyu ni balozi wa Brasil anayeongoza mkutano huo wa UNCTAD: “Kwa kweli ni makubaliano maalum. Kwanza yanahusu biashara ya mbao. Pili yanalenga pia matumizi mazuri ya misitu isiharibike ili mbao ziweze kukatwa kwa kipindi kirefu. Kwa hivyo ni zaidi kuliko makubaliano ya biashara tu. Msingi wake ni kuwezesha biashara ya mbao iende mbali.”

Maanake ni sehemu fulani ya makubaliano haya yanahusu kulinda mazingira, yaani misitu ya nchi zenye ujoto. Hata hivyo siyo makubaliano kuihifadhi misitu, kama mkuu wa shirika la kimataifa la mbao za nchi za joto, ITTO. Aya zote zinazozingatia masuala ya mazingira zinaandikwa bila kuweka sheria lakini lugha ni wazi kidogo. Badala yake shirika la ITTO linaahidi kuzisaidia nchi zinazoendelea kuneemesha namna ya kukata misitu ili ibake, pamoja na miradi maalum kuhifadhi na kudhibiti misitu ya joto.

Mashirika ya mazingira kama vile Greenpeace na Robinwood yanapinga makubaliano haya ya UNCTAD kuhusu mbao wa nchi za joto. Kwa maoni yao, mkataba kama huo hauwezi kusaidia kuhifadhi misitu katika nchi za joto, kwa kuwa yanazingatia hasa biashara na ni sehemu ndogo tu inayolenga kulinda mazingira na kuyazingatia maslahi ya makabila ya wenyeji.

Majadiliano juu ya maslahi ya mazingira kwenye upande mmoja na maslahi ya kiuchumi kwenye upande mwingine, ndiyo sababu moja kwa kuwa ni vigumu kufikia makubaliano. Tayari ni awamu ya nne inayoendelea mjini Geneva, Switzerland kwenye makao makuu ya shirika la UNCTAD. Nchi kadhaa zinazoingiza bidhaa kutoka nchi za nje kwa mfano nchi za Umoja wa Ulaya zinataka mkataba huo mpya uwe na masharti makali ya kulinda misitu ya nchi za joto. Kwa upande mwingine kuna nchi nyingi zinazotengeza mbao, kati yao pia ni nchi maskini ambazo zina maslahi tofauti kwa kuwa biashara ya mbao ina umuhimu kubwa kwao. Nchi hizi zinadai, ikiwa nchi za kiviwanda zinataka mazingira yalindwe, basi zijitolee zaidi kifedha katika miradi ya shirika la kimataifa la mbao kwa nchi za joto, ITTO inayolenga kuneemesha matumizi ya misitu ya joto.

Suala ya kugharamia miradi ndiyo tatizo kuu la ITTO, kama mkuu wake, Bw. Maoel Sobral Filho anavyosisitiza: “Asilimia 40 ya miradi yetu ambayo ilipitishwa na baraza la ITTO haijatekelezwa kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Maslahi muhimu kabisa ya nchi zinazoendelea ambazo zinatengeneza mbao ni kuhakikisha kwamba miradi yao itagharamiwa. Hilo ndilo suala muhimu katika majadiliano.”

Ikiwa washiriki watafanikiwa katika kufikia makubaliano kuhusu biashara ya mbao kutoka nchi za joto, bado ni wazi. Kulingana na mwenyekiti wa majadiliano, balozi Ranahos wa Brasil, awamu nyingine haiwezekani. Kama majadiliano yatashindwa, kifaa muhimu cha kudhibiti biashara ya mbao za nchi za joto na kuilinda misitu ya joto kitapotea.