1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Afrika wahimiza amani DRC

10 Januari 2019

Umoja wa Afrika umetoa wito kwa migogoro yoyote kuhusu matokeo ya uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kutatuliwa kwa njia ya amani na kupitia majadiliano.

https://p.dw.com/p/3BKkH
Félix Tshisekedi
Picha: Reuters/B. Ratner

Taarifa kutoka ofisi ya mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat imesema ni muhimu kwamba tofauti zozote kuhusu matokeo yaliotangazwa, kwamba hayakuakisi matakwa ya wapigakura, zitatuliwe kwa amani, kwa kutumia sheria husika na kupitia majadiliano ya kisiasa kati ya vyama vinavyohusika.

Mahamat hakumpongeza mgombea wa upinzani alishinda Felix Tshisekedi, ambaye ushindi wake umepokelewa na vilio vya udanganyifu na tuhuma kwamba alifikia makubaliano na rais anaeondoka Joseph Kabila, ambaye mgombea wake aliemteua mwenyewe ameshika nafasi ya tatu.

Äthiopien Addis Abeba Moussa Faki
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki MahamatPicha: picture-alliance/AA/M. W. Hailu

Kanisa Katoliki nchini humo limesema matokeo ya awali hayawiani na data lilizokusanya huku Ufaransa ikisema inaamini mgombea mwingne wa upinzani Martin Fayulu ndiye alieshinda kihalali.

Mahamati  alisema tu amezingatia matokeo ya awali na kusema bila kujali matokeo ya mwisho ya uchaguzi, DRC inapaswa kutafuta muafaka wa kitaifa kwa msingi wa kuheshimu kanuni za demokrasia na haki za binadamu pamoja na kulinda na kuimarisha amani.

Umoja wa Ulaya umesema unafuatilia matokeo ya kushtukiza ya uchaguzi huo na pia kutilia maanani matamshi ya waliochukua nafasi ya pili katika uchaguzi huo walioyafananisha matokeo haya na mapinduzi.

Msemaji wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Maja Kocijancic amesema kwa sasa wanasubiri ufafanuzi kutoka kwa waangalizi wa Kimataifa huku ikizitaka pande zote kujiepusha na vurugu na kuonya kuwa matokeo ya mwisho yanapaswa kuendana na matakwa ya raia wa Congo.

Südafrika - neuer Präsident Cyril Ramaphosa
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa Picha: Getty Images/AFP/M. Hutchings

Afrika Kusini imeiomba CENI kukamilisha utoaji wa matokeo kwa uaminifu na kuzingatia amani na uthabiti wa nchi.

Kwa upande wake waziri wa mambo ya nje wa Ubelgiji Didier Reynders amesema nchi yake inapanga kuliwasilisha suala la Congo katika Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ambapo ubelgiji imekuwepo kwa miaka miwili sasa.

Afrika kusini nayo imeiomba tume ya kitaifa ya uchaguzi CENI kukamilisha utoaji wa matokeo na kuhakikisha uaminifu na kuzingatia amani na uthabiti wa nchi.

Rais Cyril Ramaphosa ameipongeza Congo kwa kuandaa uchaguzi na kutoa wito kwa mataifa ya maeneo na jamii ya kimataifa kujizuwiya na dhana na kuwaacha maafisa wa tume ya uchaguzi kumaliza kazi yao.

Mwandishi:  Amina Abubakar/AFP/AP

Mhariri: Iddi Ssessanga