1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama ya katiba yakosoa mageuzi ya uchaguzi Ujerumani

Sylvia Mwehozi
30 Julai 2024

Mahakama ya kikatiba ya shirikisho mjini Karlsruhe nchini Ujerumani, imeamua kuwa sehemu ya mageuzi ya uchaguzi yanayolenga kupunguza ukubwa wa bunge nchini Ujerumani, yanakwenda kinyume na katiba.

https://p.dw.com/p/4iuvV
Karsruhe | Mahakama ya katiba ya shirikisho
Majaji katika mahakama ya katiba mjini Karsruhe Picha: Uli Deck/dpa/picture alliance

Mageuzi hayo yaliyoratibiwa na muungano tawala wa Kansela Olaf Scholz yanalenga kuweka ukomo wa viti katika bunge la Ujerumani la Bundestag kufikia viti 630 kutoka idadi ya sasa ya viti 736. Bunge hilo la Ujerumani linazingatiwa kuwa ndio bunge kubwa zaidi duniani ambalo limechaguliwa kidemokrasia.

Nchini ujerumani, kuna mfumo mgumu wa uchaguziunaozingatia zaidi kutowa nafasi ya chama kupata uwakilishi wa viti bungeni, pale kitakapofanikiwa kupata asilimia 5 ya kura kitaifa, mfumo ambao unaruhusu idadi ya wabunge kuongezeka kutegemea na matokeo ya uchaguzi.

Kiongozi wa chama cha CSU Markus Söder
Kiongozi wa Bavaria Markus Söder kutoka chama cha CSUPicha: Bernd Elmenthaler/Geisler-Fotopress/picture alliance

Kwa kawaida, Wajerumani hupiga kura mbili katika uchaguzi wa bunge la kitaifa. Kura ya kwanza ni ya mwakilishi wa kikanda au kimkoa na ya pili ni kwa chama wanachokipendelea ambayo ndio inaamua uimara wa chama bungeni.

Soma zaidi: Mfumo wa uchaguzi wa Ujerumani

Ili vyama viweze kuingia bungeni, vilipaswa kupata asilimia 5 ya kura za nchi nzima. Mageuzi hayo yalikusudia kubadili mfumo huo ambao ulikuwa ukivinufaisha vyama vidogo kuweza kuingia bungeni kupitia kura za moja kwa moja za mgombea katika majimbo hata kama havikupata asilimia 5 ya kura za nchi nzima.

Uchaguzi uliopita wa Ujerumani: Ujerumani yaamua

Hata hivyo mahakama ya kikatiba ya shirikisho ya mjini Karlsruhe imesema kipengele hicho ambacho kilianzishwa mwaka 2023 na kingeanza kutumika katika uchaguzi wa bunge wa mwakani ni kinyume na katiba.

Chama cha mrengo wa kushoto cha Die Linke na kile cha Kihafidhina cha Bavaria,Christian Social Union,CSU ambavyo kwa kawaida havikubaliani kisiasa katika masuala mengi, kwa pamoja vilichukua hatua za kisheria dhidi ya mageuzi hayo,yaliyopendekezwa na kundi la serikali inayoongozwa na kansela Scholz, kwasababu yangeviathiri vyama vidogo zaidi au vile vya kikanda.

Kwa nyongeza ni kwamba zaidi ya wananchi 4,000 wamewasilisha mapingamizi ya kikatiba yaliyotokana na haki sawa za kupiga kura na haki ya kupata fursa sawa kwa vyama vya siasa.

Ujerumani: CSU yapoteza uongozi wa Bavaria

Chama cha Christian Social Union CSU cha Bavaria na kile cha Die Linke ndio vilikuwa njiapanda kutokana na kwamba mfumo wa wagombea wa moja kwa moja ndio unawawezesha kuingia bungeni.

Katika uchaguzi wa shirikisho wa mwaka 2021, CSU ambacho kiko tu Bavaria, kilipata asilimia 5.2 ya kura za chama nchi nzima. Kama kingepata chini ya asilimia 5 ya kura za nchi nzima katika uchaguzi ujao ingemaanisha kwamba kingetupwa nje ya bunge chini ya sheria hiyo mpya hata kama kingeshinda kura za moja kwa moja za majimbo huko Bavaria.

Waziri mkuu wa Bavaria na kiongozi wa CSU Markus Söder, amekaribisha uamuzi huo, akisema "ni mafanikio ya wazi ya CSU na Bavaria na pia ni pigo kwa serikali ya muungano tawala."

Ama kwa upande mwingine chama cha Kansela Scholz cha Social Democratic SPD pia kimeutaja uamuzi huo kuwa ni ushindi haswa suala la kupunguza ukubwa wa bunge ambalo mahakama imeutaja kuwa ni sawa kikatiba.