1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama ya Kimataifa ya ICC yakanusha taarifa za kutoa kibali, kukamatwa Rais wa Sudan.

Halima Nyanza/DPA/Reuters12 Februari 2009

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ya Mjini The Hague, imekanusha kwamba imefikia maamuzi ya kutoa kibali cha kukamatwa kwa Rais Omar Hassan Al Bashir wa Sudan, kuhusika na uhalifu wa kivita jimboni Darfur.

https://p.dw.com/p/GsMI
Pichani, Rais wa Sudan Omar Hassan Al-Bashir, ambaye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita, imekanusha kutoa waranti wa kumkamata.Picha: AP

Kukanusha taarifa hiyo kulikotolewa na mahakama hiyo kunafuatia ripoti zilizotolewa na gazeti la New York Times jana, kwamba Majaji katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita mjini The Hague Uholanzi, wamefikia maamuzi ya kutoa kibali cha kukamatwa kwa Rais wa Sudan, Omar Hassan Al Bashir.


Habari hizi za kutolewa kwa Waranti huo wa kukamatwa Rais wa Sudan imeripotiwa katika mtandao wa gazeti hilo, likidai kuwanukuu mawakili na wanadiplomasia wa mahakama hiyo.


Msemaji wa Mahakama hiyo ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita, Laurence Blairon amesema kwa sasa hakuna kibali kilichotolewa na kama wanakitu watatangaza.


Naye Msemaji wa Umoja wa Mataifa Marie Okabe amekanusha ripoti zilizotolewa na gazeti hilo kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon, amearifiwa na Mahakama hiyo ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita kwamba kwamba kibali hicho cha Kukamatwa Rais Omar Hassan Al Bashir wa Sudan kimetolewa.


Akizungumza jana jioni Bi Marie Okabe amesema hakuna maamuzi yoyote yaliyopokelewa na Katibu Mkuu kuhusiana na suala hilo na kwamba hawatarajii kupokea kutokana na kwamba kwa kawaida hawapokei maamuzi ya mahakama.


Katika hatua nyingine Sudan nayo imedharau ripoti hizo zilizotolewa za kutolewa hati ya kukamatwa kwa Rais wa nchi hiyo kwa kuiusema kuwa inaendelea na hatua zake za kidiplomasiakuweza kuahirisha suala hilo.


Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje wa Sudan,imearifu pia kwamba haijapokea taarifa yoyoyte kutoka mahakama hiyo ya The Hague kuhusiana na suala hilo.


Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje wa Sudan Ali al Sadiq amesema ni lazima wasubiri tangazo kutoka katika mahakama hiyo na kusema kuwa wajumbe kutoka Umoja wa Afrika na Jumuia ya kiarabu kwa sasa bado wanalifanyia kazi suala hilo, ikiwemo pia China na Urusi na hivyo kwa sasa ni mapema mno kuzunguzia suala hilo.


Siku ya Jumatatu msemaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita ICC, mjini The Hague alisema kuwa watafikia uamuzi wa kutoa waranti hiyo wiki hii, lakini hakutaja jina ni siku gani.


Waranti ya kukamatwa kwa Rais huyo wa Sudan ilitokana na ombi lililotolewa mwezi Julai na Mwendesha mashtaka mkuuu wa Mahakama hiyo ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita Luis Moreno-Ocampo kwa tuhuma za mauaji ya halaiki, uhalifu dhidi ya ubinadamu katika jimbo la magharibi la Sudan la Darfur, ambako kumekuwa na mzozo wa kikabila tangu mwaka 2003.


Waranti huo utakuwa ni wa kwanza kutolewa na mahakama hiyo, kwa mkuu wa nchi.


Kwa upande wake Balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa AbdalMahmoud Abdal Haleem ameelezea uwezekano huo wa kutolewa kibali cha kukamatwa kwa Rais Bashir ni tusi kwa Sudan.


Umoja wa Afrika na Wanadiplomasia katika nchi za Kiarabu tayari wameonya kuwa jaribio hilo la kumshtaki Rais huyo wa Sudan, litasababisha utata katika mpango wa amani wa Darfur.


Katika hatua nyingine Kiongozi wa kundi la waasi wa Darfur la Justice and Equality Movement Khalil Ibrahim pamoja na Kiongozi wa Ujumbe wa Serikali ambaye pia ni msaidizi wa Rais Nafie Ali Nafie wamekutana katika mazumnguzo yao ya kwanza ya moja kwa moja katika mji mkuu wa Qatar Doha, wenye lengo la kufikia suluhisho la kisiasa katika mzozo wa eneo hilo la magharibi mwa Sudan.