1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUganda

Uganda: Korti yafuta kifungu tata cha sheria ya mawasiliano

10 Januari 2023

Korti nchini Uganda imeifuta sehemu ya sheria ya mawasiliano iliyokuwa ikitumika kuwashtaki wakosoaji wa serikali, waandishi wa habari wakiwemo waliokimbilia uhamishoni Ujerumani Stella Nyanzi na Kakwenza Rukirabashaija.

https://p.dw.com/p/4Ly11
Symbolbild | Justiz
Picha: fikmik/YAY Images/IMAGO

Katika uamuzi wa shauri lililowasilishwa na mwanaharakati anayetaka kufutwa kwa kifungu hicho cha sheria, Mahakama ya Kikatiba nchini Uganda ilikubaliana na ombi hilo, kwa kusema sheria hiyo ilikiuka katiba.

Jaji wa mahakama ya Katiba nchini humo Kenneth Kakuru, aliyeuandika kwa niaba ya jopo la majaji watano, uamuzi wa kuifuta sehemu hiyo ya sheria ya mawasiliano, ameweka bayana kuwa sheria hiyo "haikubaliki kwa kuwa inabinya uhuru wa kujieleza katika jamii huru na ya kidemokrasia."

Jaji Kakuru ameitaja sheria hiyo kuwa ni batili na amepiga marufuku utekelezaji wake.

Soma pia: Uganda yamkamata mshukiwa wa mkanyagano wa mwaka mpya

Msemaji wa serikali Ofwono Opondo hakujibu ombi la shirika la habari la Reuters lililomtaka atoe tamko juu ya uamuzi huo.

Chini ya kifungu cha matumizi mabaya ya sheria ya mawasiliano, moja ya kipengee katika sheria hiyo inakataza matumizi ya mawasiliano kwa njia ya kieletroniki ili "kuvuruga amani, utulivu au haki ya faragha ya mtu yeyote bila ya kusudio la kufanya mawasiliano kwa njia halali."

Kwa kawaida, wanakiuka sheria hiyo hukabiliwa na adhabu mbalimbali ikiwemo faini ya pesa taslimu ama kifungo cha miaka kadhaa gerezani.

Stella Nyanzi
Mhadhiri na mwandishi ambaye ni mkosoaji wa Rais Yoweri Museveni, Stella NyanziPicha: Konrad Hirsch

Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamikia sheria za mawasiliano za Uganda zilizowekwa na serikali ya Rais Yoweri Museveni.

Soma pia: Agizo la Museveni lazua mshangao Uganda

Wakosoaji wameeleza kuwa sheria hizo ni za kibaguzi, na kwamba zimekuwa zikitumika kuwaadhibu wapinzani wa Museveni, ambaye ameitawala nchi hiyo ya Afrika Mashariki tangu mwaka 1986.

Stella Nyanzi, mhadhiri wa chuo kikuu ambaye pia ni mwandishi aliyejizolea umaarufu mkubwa katika mitandao ya kijamii kutokana na ukosoaji wake wa serikali ya Museveni, alitupwa gerezani kwa zaidi ya mwaka mmoja baada ya kukutwa na hatia chini ya sheria ya mawasiliano ya Uganda.

Nyanzi hatimaye alifanikiwa kuikimbia Uganda na sasa anaishi uhamishoni hapa Ujerumani pamoja na mwandishi mwengine wa kuko huko Uganda- mshindi wa tuzo ya kimataifa Kakwenza Rukirabashaija, ambaye pia alishtakiwa chini ya kifungu hicho cha sheria ya mawasiliano kabla ya yeye pia kukimbia.