1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hakuna karantini Uganda kwa ajili ya kudhibiti Ebola

29 Septemba 2022

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameondoa wasiwasi kwa umma uliodhani angetangaza hatua za karantini katika hatua za kudhibiti mlipuko wa ugonjwa hatari wa Ebola.

https://p.dw.com/p/4HUWv
EAC Staaten Video-Konferenz | Yoweri Museveni
Picha: Philbert Rweyemamu/EAC

Rais Museveni akilihutubia taifa usiku wa kuamkia leo Alhamisi, kiongozi huyo amelezea kuwa hapana haja ya kuweka vizuizi kwa sababu ameona pana urahisi kudhibiti maambukizi ya Ebola ikilinganishwa na maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID-19.

Kambi ya kuwatibu wagonjwa wa Ebola katika eneo la Mubende nchini Uganda.
Kambi ya kuwatibu wagonjwa wa Ebola katika eneo la Mubende nchini Uganda.Picha: BADRU KATUMBA/AFP via Getty Images

Kiongozi huyo wa Uganda amesema kwenye hotuba yake kwamba kulingana na takwimu za wizara ya afya ni watu watano ndiyo wamethibitishwa kufariki kutokana na mlipuko wa Ebola tangu wizara hiyo ilipotangaza rasmi kwamba ugonjwa huo umegunduliwa nchini Uganda. Waathirika kwa jumla ni 31 na kwamba kwa sasa idadi kubwa ya waathirika wamo katika wilaya tatu zilizo jirani.

Shirika la Afya Ulimwenguni WHO limesema ugonjwa wa Ebola ulionazia Sudan umeonesha kuwa hauambukizi kwa kasi na pia kiwango cha vifo ni cha chini tofauti na milipuko ya hapo awali uliotokea nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambapo karibu watu 2,300 walikufa mnamo mwaka 2018hadi mwaka 2020. Huko nchini Uganda maambukizi ya hivi karibuni yalizuka katika wilaya ya Mubende katikati mwa Uganda, karibu kilomita 150 magharibi mwa mji mkuu Kampala na tangu wakati huo yameenea katika wilaya mbili zaidi.

Mfanyakazi wa afya katika hospitali ya wilaya ya Mubende nchini Uganda.
Mfanyakazi wa afya katika hospitali ya wilaya ya Mubende nchini Uganda.Picha: Nicholas Kajoba/Xinhua News Agency/picture alliance

Habari za kutokuwepo kwa hatua za karantini hata katika maeneo kulikogunduliwa wagonjwa wa ebola zimepokelewa kwa afueni kubwa na wananchi. Ila pia imedhihirika kuwa watu wengine hawakuwa na habari kuhusu mlipuko huu hali inayomaanisha kwamba hapajakuwa na uhamasishaji wa kutosha.

Hata hivyo wadau katika biashara mbalimbali wamelezea mashaka iwapo watu waliokuwa wamepanga kwenda nchini Uganda kama watalii wataridhika na kushawishika kwamba hakuna tishio kubwa kutokana na mripuko wa Ebola nchini humo na hivyo kuendelea na mipango yao ya safari. Rais Museveni amefafanua kuwa amefanya maamuzi hayo kwa ushauri wa wataalamu wa afya na wanasayansi na amewaaambia raia wake kwamba ni rahisi kuepusha maambukizi ya Ebola ikiwa watazingatia usafi wa mwili na kwenye maeneo yao na kuwahimiza kuosha mikono mara kwa mara.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni
Rais wa Uganda Yoweri MuseveniPicha: ABUBAKER LUBOWA/REUTERS

Waziri wa afya wa Uganda Jane Ruth Aceng pia amelezea hayo hayo na amewahimiza wafanyakazi wa afya kuzingatia zaidi kuvalia vifaa kinga kama njia mojawapo ya kuepusha maambukizi kutoka kwa wagonjwa.

Vyanzo:AFP7RTRE