1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama ya ICC yaadhimisha miaka 20 ya uwepo wake

Zainab Aziz Mhariri:Yusuf Saumu
1 Julai 2022

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC leo imeadhimisha miaka 20 tangu kuundwa kwake. Vita vya Ukraine na Urusi vinaipa mahakama hiyo msukumo mpya baada ya miongo miwili ya utata na kukosolewa.

https://p.dw.com/p/4DXMM
Niederlande ICC Gebäude Den Haag
Picha: Peter Dejong/AP Photo/picture alliance

Waendesha mashtaka wanachunguza uhalifu wa kivita katika nchi mbalimbali duniani, ikiwa ni pamoja na uchunguzi unaoihusu Ukraine ambao mtaalamu mmoja ameuita kuwa ni uchunguzi wa  "kujenga au kubomoa". 

Mahakama hiyo, imekosolewa kwa muda mrefu kwa kushughulikia uhalifu wa barani Afrika pekee na kushindwa kuwapata na hatia viongozi wakuu wa nchini Kenya na Ivory Coast. Mahakama hiyo ya uhalifu wa kivita sasa inaendeleza uchunguzi katika nchi 17, kutokea Afghanistan hadi Ukraine, ingawa nyingi ya kesi zinazochunguzwa ni za katika bara la Afrika tu.

David Crane, mwendesha mashtaka wa Mahakama Maalum kwa ajili ya Sierra Leone ambayo ilimtia hatiani Rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor na watu wengine kwa makosa ya uhalifu wa kivita, amesema mahakama ya ICC yenye makao yake mjini The Hague ni taasisi muhimu ya kisheria licha ya baadhi ya kazi zake kukosolewa.

Katikati: Rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor
Katikati: Rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor Picha: Rob Keeris/AFP/Getty Images

Crane ameliambia shirika la Habari la AP kwamba kwa uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, mahakama ya ICC lazima iwe mstari wa mbele katika kumwajibisha Rais Vladimir Putin. Mahakama ya uhalifu wa kivita imekamilisha mashtaka matatu pekee ya uhalifu wa kivita na mengine matano yanayohusu kuingilia haki katika kipindi cha miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Mkataba wa Roma, ulioanza kutumika Julai mosi, mwaka 2002.

Haina jeshi lake la polisi na hivyo wakati wote mahakma hiyo inategemea mamlaka za kitaifa kubeba jukumu la kuwakamata, na kuwafikisha washukiwa katika mahakama hiyo mjini The Hague hali ambayo kutoka mwanzo limekuwa ni tatizo na kuna uwezekano wa tatizo hilo kubaki kuwa kikwazo kikubwa katika utekelezaji wa haki.

David Crane, mwendesha mashtaka wa ICC amesema kupatikana kwa haki hiyo hakuna unafuu kwani bajeti ya mahakama ya mwaka 2022 ni karibu euro milioni 155, na mpaka sasa mahakama hiyo imetumia zaidi ya euro bilioni 2.2 katika muda wa miongo miwili.

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Karim Asad Ahmad Khan
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Karim Asad Ahmad KhanPicha: Marwan Ali/AP/picture alliance

Jumla ya nchi 123 ni wanachama wa mahakama hiyo ya ICC na zinaunga mkono mamlaka yake, lakini nchi za kimataifa kama Marekani, Urusi na China haziitambui mahakama ya ICC. Hiyo ina maana kwamba kama uchunguzi wa Mwendesha Mashtaka mkuu wa ICC, Karim Khan kuhusu Ukraine utaamua kuwafungulia mashtaka watuhumiwa ambao ni raia wa Urusi, bila shaka Moscow haitatoa ushirikiano wa kuwapeleka raia wake kwenda kujibu mashtaka katika mahakama ya mjini The Hague.

Maadhimisho ya siku ya leo Ijumaa yanapaswa kuwa ni wakati wa kutafakari na kujaribu kurudisha upya mchakato wa haki ya kimataifa, amesema mwendesha mashta mkuu Karim Khan. Katika taarifa yake juu ya maadhimisho hayo, Umoja wa Ulaya umeangazia mafanikio ya mahakama ya ICC na umetoa wito kwa mataifa ambayo bado hayajajiunga kufanya hivyo mara moja.

Vyanzo:AP/AFP