1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha AfD chatajwa kuwa ni kundi la itikadi kali.

13 Mei 2024

Mahakama ya juu ya jimbo la NorthRhine Westphalia, iliyoko mjini Münster, imetoa uamuzi unaokiweka chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AfD katika orodha ya makundi yanayoshukiwa kuwa ya itikadi kali.

https://p.dw.com/p/4fmz4
Deutschland | Berufungsverfahren zu  Einstufung der AfD durch Verfassungsschutz
Picha: Guido Kirchner/dpa/picture alliance

Idara za ujasusi za Ujerumani kwa muda sasa zimekitaja chama hicho pamoja na tawi lake la vijana kuwa makundi yanayoshukiwa kuendesha itikadi kali za kisiasa za mrengo wa kulia.

Uamuzi wa mahakama ya juu iliyoko mjini Münster umetolewa leo Jumatatu na ni uamuzi unaofuatia kesi ya rufaa iliyopelekwa na chama hicho cha AfD kupinga uamuzi wa kwanza ulitolewa na mahakama ya chini mjini Cologne,uliosema chama hicho kinapaswa kuendelea kutazamwa kama kundi la itikadi kali linalotakiwa kufuatiliwa.

Mahakama ya Cologne ilitowa uamuzi wake huo mwaka 2022  ikiunga mkono ripoti za idara za ujasusi na kutowa kibali cha kuendelea kufuatiliwa chama hicho.

Bango la chama cha AfD Münster
Alama ya chama cha AfDPicha: Rolf Haid/picture alliance

Uamuzi wa Mahakama ya Juu

Sasa uamuzi uliotolewa leo na mahakama ya juu ya jimbo la NorthRhine Westphalia umeunga mkono uamuzi huo uliotolewa mwanzo na kusema AfD pamoja na tawi lake la vijana linalofahamika kama Junge Altenative(JA) linaweza kutazamwa kama washukiwa wa mitizamo ya  itikadi kali.

Hata hivyo uamuzi huo bado hauna mamlaka ya kisheria kwasababu chama hicho kinaweza bado kuwasilisha ombi lake la rufaa mbele ya mahakama ya shirikisho mjini Leipzig.

Chama cha AfD kinafahamika kuwa chama chenye misimamo ya kupinga wageni nchini Ujerzmani na kinajiimarisha kutokana na kuongezeka kwa wasiwasi miongoni mwa wapiga kura wakijerumani kufuatia kuongezeka kwa idadi ya watu wanaotafuta hifadhi ya ukimbizi nchini Ujerumani.

Ukweli wa mambo ni kwamba kufikia sasa chama hicho kinachowachukia wageni kinaungwa mkono na kiasi asilimia 20 kitaifa  kutokana na kuwepo hali ya wananchi wengi kutoridhishwa na serikali ya mseto inayoongozwa na Kansela Olaf Scholz.

Kesi ya AfD ikifuatiliwa
Wafuatiliaji wa kesi ya AfD Picha: Guido Kirchner/dpa/picture alliance

Uamuzi wa mahakama ya juu mjini Münster unavipa ruhusu vyombo vya usalama kufuatilia nyendo zote za chama hicho na tangu mwaka 2021 taasisi ya shirikisho yenye jukumu la kuilinda katiba ya nchi BfV na ambayo inalinda utaratibu wa demokrasia ya taifa hili dhidi ya vitisho vya makundi ya siasa kali, iliikiorodhesha chama hicho cha AfD kama kundi lenye uwezekano wa kuendeleza itikadi na siasa kali.

Mahakama yasema imepokea ushahidi wa kutosha 

Mahakama ya Münster imesema kuna ushahidi wa kutosha kwamba chama hicho  kinaendeleza malengo yanayokwenda kinyume na utu wa binadamu kuelekea makundi fulani ya watu na dhidi ya Demokrasia.

Mahakama hiyo imebaini kuwepo kwa misingi ya kushuku alau sehemu ya chama hicho kwamba inataka kuwafanya raia wa Ujerumani wenye asili ya kigeni kuwa watu wa daraja la pili.

Chama hicho ambayo kimejiongezea umaarufu katika majimbo mengi ya Mashariki mwa Ujerumani ambayo yatafanya uchaguzi baadae mwaka huu, hivi karibuni kimekuwa kikifuatiliwa kwa kiasi kikubwa kutokana na kauli za kibaguzi zinazotolewa na wanachama wake lakini pia kufuatia tuhuma kwamba kinawahifadhi mashushu wanaozitumikia   Urusi na China.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW