1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Khofu yaongezeka Ujerumani kuhusu umaarufu wa chama cha AfD

17 Januari 2024

Maelfu ya Wajerumani wafanya maandamano katika miji mbali mbali kukipinga chama cha siasa kali kisichopenda wageni

https://p.dw.com/p/4bMKX
Wajerumani waandamana kupinga siasa kali za AfD
Maandamano ya mjini BerlinPicha: Bernd Elmenthaler/Geisler-Fotopress/picture alliance

Wasiwasi umeongeza nchini Ujerumani kuhusu kupata nguvu kwa chama cha siasa kali  kisichopenda wageni cha Alternative für Deutschland,yaani chama mbadala kwa Ujerumani..

Zaidi ya watu 10,000 walijiunga na maandamano mjini Kolon kukipinga chama hicho ambacho sasa kinafungamanishwa na makundi ya wenye itikadi kali za kizalendo.

Maelfu walijitokeza jana Jumanne katikati ya mji wa Kolon kushiriki maandamano ya kukipinga chama cha AfD,wakiwa wamebeba mabango yaliyoandikwa ujumbe unaosema Ujerumani ni nchi ya watu mchanganyiko, na ndio waliowengi kuliko AfD inayotaka kutengeneza njia ya kuwepo ufashisti Ujerumani. Baadhi ya Wajerumani wanasema chama hicho cha siasa kali kinawakumbusha utawala wa  Kinazi.

Maelfu waliojitokeza Postdam
Maandamano ya PostdamPicha: Sebastian Christoph Gollnow/dpa/picture alliance

''Wanasiasa wanaojinasibisha na siasa kali za mrengo wa kulia wanapaswa kukabiliwa na kudhibitiwa bungeni.Wanapaswa kushtakiwa mahakamani''

''Vyombo vya habari vinavyojitegemea kama ,kituo cha habari za uchunguzi cha Correctiv hatimae kimeichapisha hii habari na hilo linapaswa kueleweka kwa watu wote kwamba namna mambo yanayovyokwenda yanaelekea pabaya na kila mmoja inabidi kwa kweli ajitokeze kuandamana.''

Khofu imeongezeka zaidi miongoni mwa Wajerumani kuelekea misimamo ya chama hicho baada ya hivi karibuni kufichuka ripoti kwamba maafisa wa AfD walikuwa na mkutano na kundi la watu wanaopigania sera za kuwafukuza watu wote wasiokuwa na asili ya Ujerumani. Inaelezwa kwamba mkutano huo ulifanyika mwezi Novemba mwaka jana.

Ufichuzi huo ulitolewa na kituo kimoja cha habari kinachoitwa Correctiv,kikisema kwamba viongozi chungunzima waandamizi wa AfD walikutana na wenye itikadi kali za kisiasa katika mji wa Postdam akiwemo Martin Sellner,mtu ambaye ni raia wa Austria,na kiongozi wa muda mrefu wa vuguvugu la mrengo wa siasa za chuki dhidi ya wahamiaji wakiislamu barani Ulaya.

Wabunge wa chama hicho wamepuuza ufichuzi huo huku ikielezwa kwamba wanapanga kujadili suala hilo ndani ya chama chao katika kipindi cha siku kadhaa zijazo. Makamu wa Kansela Robert Habeck amesema wanachama wa AfD  ni waimla wanaohatarisha  mwelekeo wa kidemokrasia nchini Ujerumani.

Maandamano dhidi ya wanaoitwa Wanazi mjini Berlin
Wajerumani wakipinga chama cha AfdPicha: Michael Kuenne/ZUMAPRESS/picture alliance

Ikumbukwe kwamba chama cha AfD kimeongeza umaarufu wake nchini Ujerumani kikizidi kuungwa mkono kwa mujibu wa utafiti wa maoni ya kitaifa na kimajimbo na inatajwa kwamba huenda kikaibuka kuwa chama kikubwa zaidi katika chaguzi zijazo kwenye majimbo matatu upande wa iliyokuwa Ujerumani Mashariki,zitakazofanyika mwezi Septemba mwaka huu.

Katika maandamano ya mjini Kolon mwandishi habari wa shirika la habari la Ujerumani Dpa  anasema maandamano yalifanyika kwa njia ya amani  huku ukipigwa muziki na bendera za Umoja wa Ulaya zikipeperushwa pamoja na mabango yaliyochorwa rangi za upinde wa mvua.

Moja ya Mabango lilikuwa na ujumbe unaowafanyia matashtiti wasiopenda wageni nchini Ujerumani,ujumbe huo ulisema,''Manazi wanakula mikate ya Doner kwa siri siri''.

Waandamanaji mjini Köln
Maandamano ya KölnPicha: Marc John/IMAGO

Kimsingi mikate hiyo ya Doner ni maarufu nchini Ujerumani na asili yake ni Uturuki na inapikwa hasa na Waturuki.Waandamanaji pia walikuwa wakipaza sauti wakiitaka serikali na bunge wafikirie kukipiga marufuku chama cha AfD.

Tayari chama hicho kinafuatiliwa na idara za Ujasusi nchini Ujerumani. Maandamano yalifanyika pia jana katika mji wa Kaskazini mwa Ujerumani wa Schwerin kupinga kuongezeka kwa nguvu za AfD. Mwishoni mwa Juma miji kadhaa ya Ujerumani pia yalishuhudia maandamano kama hayo.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW