1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelfu ya wakulima na matrekta yao kuandamana mjini Berlin

15 Januari 2024

Maelfu ya wakulima nchini Ujerumani wanatazamiwa kufanya maandamano makubwa mjini Berlin, ikiwa ni kilele cha maandamano yaliyodumu kwa wiki nzima kuishinikiza serikali kutoondoa nafuu za kikodi kwenye sekta ya kilimo.

https://p.dw.com/p/4bEf0
Ujerumani, Berlin | Maandamano ya wakulima Brandenburg
Maelfu ya Matrekta yakiwa yamepangwa mbele ya lango maarufu la Brandenburg mjini Berlin ikiwa ni sehemu ya maandamano ya wakuliwa nchini Ujerumani.Picha: Nadja Wohlleben/REUTERS

Kutwa nzima ya jana Jumapili, wakulima kutoka kila pembe ya Ujerumani walikuwa wanaelekea mjini Berlin ambako inaaminika zaidi ya matrekta 3,000 na malori 2,000 yataingizwa katikati ya mji.

Maandamano ya leo yanapangwa kufanyika mbele ya lango mashuhuri la Brandenburg na watu wapatao 10,000 wengi wakiwa ni wakulima wanatarajiwa kuhudhuria.

Maandamano hayo yaliyoanza Jumatatu iliyopita yameongeza shinikizo kwa serikali ya mseto ya Kansela Olaf Sholz ambayo bado inahangaika kutatua mzozo kuhusu bajeti ya mwaka ujao.

Shinikizo la wakulima limeilazimisha serikali kufutilia mbali mipango ya kuondoa nafuu ya kodi kwenye vyombo vya moto vinavyotumika kwa kilimo pamoja na kupendekeza kuondoa kwa awamu ruzuku inayotolewa na serikali kwenye mafuta ya Dizeli yanayoendesha mitambo mashambani.