1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaVenezuela

Maelfu waandamana Venezuela kupinga ushindi wa Rais Maduro

30 Julai 2024

Vikosi vya usalama nchini Venezuela vimetumia mabomu ya machozi na risasi za mpira kuwatawanya waandamanaji walioingia mitaani kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi rais Nicolas Maduro.

https://p.dw.com/p/4ispN
Polisi wakishika doria wakati watu wakikusanyika kufanya maandamano ya kupinga ushindi wa Rais Nicolas Maduro
Polisi wakishika doria wakati watu wakikusanyika kufanya maandamano ya kupinga ushindi wa Rais Nicolas Maduro.Picha: Pedro Rances Mattey/Anadolu/picture alliance

Matokeo hayo ya uchaguzi wa siku ya Jumapiliyanapingwa na upande wa upinzani na yametiliwa mashaka na mataifa kadhaa ya kigeni.

Maelfu ya waandamanaji walimiminika kwenye mitaa ya mji mkuu, Caracas, wakipiga mayowe ya kudai haki huku wakiapa serikali ya Maduro ni lazima iangushwe.

Baadhi yao walichana mabango ya kampeni yenye picha za Maduro na kisha kuyachoma moto. Sanamu mbili za Hugo Chavez, kiongozi wa zamani wa kisoshalisti ambaye aliiongoza nchi hiyo kwa zaidi ya muongo mmoja na kumteua Maduro kuwa mrithi wake, ziliangushwa na waandamanaji.

Shirika la Habari la AFP limeripoti kushuhudia maafisa wa usalama wakifyetua mabomu ya machozi na risasi za mpira dhidi ya waandamanaji. Baadhi ya waandamanaji walijibu kwa kuwashambulia kwa mawe.

Maandamano yameripotiwa pia kwenye vitongoji vya wakaazi masikini ambavyo ndiyo vimekuwa ngome ya Maduro na serikali yake ya kisoshalisti.

"Tunataka uhuru. Tunataka Maduro aondoke. Maduro ondoka! amesema Marina Sugey, mkaazi wa maeneo duni alipozungumza na AFP.

Maduro aidhinishwa rasmi, upinzani wasema mgombea wao ndiye rais ajaye

Rais Nicolas Maduro akihutubia wafuasi wake mjini Caracas
Rais Nicolas Maduro akihutubia wafuasi wake mjini Caracas. Picha: Fernando Vergara/AP/dpa/picture alliance

Licha ya yote hayo, hapo jana Maduro alihudhuria halfa iliyoandaliwa na tume ya uchaguzi ambayo ilimpa cheti cha ushindi unaorefusha utawala wake kwa muhula wa tatu wa miaka 6.

Hata hivyo upinzani umesema asilimia 51.2 ya kura ambazo tume imesema Maduro alipata ni za udanganyifu na kwamba mgombea wao ndiye mshindi.

Maduro mwenyewe amepuuza ukosoaji wa kimataifa na kutilia kwao shaka matokeo ya uchaguzi akisema Venezuela imekuwa ikilengwa kwa dhamira ya kuchochea mapinduzi ya kijeshi kwa lengo na kuondoa utawala unaowatetea wananchi.

Lakini kiongozi wa upinzani Maria Corina Machado aliwaambia waandishi habari kwamba matokeo walio nayo mkononi yanaonesha mgombea wa upinzani Edmundo Gonzalez Urrutia ndiye mshindi na rais ajaye wa Venezuela.

Mwanasiasa huyo aliteuliwa kupeperusha bendera ya upinzani baada ya Machado kuzuiwa na mahakama kuwania nafasi yoyote ya umma.

Kwa maelezo yake, Machado amesema mgombea wa upinzani amepata kura milioni 6.27 dhidi ya milioni 2.75 pekee za Maduro. Matokeo hayo ni toafauti na yale yaliyotangazwa na tume yaliyompa asilimia 44.2 mgombea wa upinzani.

Mataifa jirani yaanza kuutenga utawala wa Maduro baada ya matokeo ya uchaguzi 

Uchaguzi wa rais Venezuela| Caracas
Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Venezuela María Corina Machado (kulia) na mgombea wa kiti cha urais kupitia tiketi ya upinzani Edmundo González Urrutia, wakizungumza na waandishi habari kupinga ushindi wa Rais Maduro. Picha: Jeampier Mattey/dpa/picture alliance

Katika hatua nyingine, ukosoaji wa kimataifa umeendelea kuiandama Venezuala baada ya matokeo hayo ya uchaguzi.

Serikali ya Peru imewaamuru wanadiplomasia wa Venezuela kuondoka nchini humo ndani ya muda wa saa 72 baada ya tume ya uchaguzi ya Venezuela kumtangaza Rais Nicolas Maduro kuwa mshindi wa uchaguzi wa siku ya Jumapili.

Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Peru imesema imechukua hatua hiyo kwa kile ilichosema kuwa kujibu uamuzi wa makusudi wa serikali ya Venezuela wa kupindua matwaka ya umma katika uchaguzi.

Taifa jingine la Amerika ya Kusini la Uruguay kupitia waziri wa mambo ya kigeni Omar Paganini limesema serikali haitomtambua Maduro kuwa mshindi wa uchaguzi.

Viongozi wenyi wa mataifa jirani ya Amerika ya Kati na Kusini wameyapinga matokeo ya uchaguzi wakisema yamekosa uwazi.

Jumuiya ya Nchi za Amerika itafanya mkutano wa dharura siku ya Jumatano kujadili kilichotokea Venezuela na hatua za pamoja za kuchukua.