1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron na Bin Salman kupunguza athari za vita Ukraine

29 Julai 2022

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman wamekubaliana kufanya kazi pamoja ili kupunguza athari za vita nchini Ukraine, wakati wa mazugumzo mjini Paris.

https://p.dw.com/p/4Erkj
Kronprinz von Saudi-Arabien in Frankreich
Picha: Lewis Joly/AP Photo/picture alliance

Taarifa ya ofisi ya rais wa Ufaransa imesema rais Macron na Mwanamfalme wa Saudia wametilia mkazo haja ya kufikisha mwisho mzozo huo na kuongeza ushirikiano wao ili kupunguza athari zake barani Ulaya, Mashariki ya Kati na dunia kwa ujumla.

Wasaidizi wa rais wa Ufaransa waliasharia kabla ya mazungumzo hayo kwamba Macro alipanga kuiomba Saudi Arabia kuongeza uzalishaji wa mafuta kusaidia kupunguza bei za mafuta ghafi, lakini taarifa hiyo haijagusia moja kwa moja mafuta au gesi, ikisema tu kwamba Macron ametilia mkazo umuhimu kuendelea na ushirikiano uliopo na Saudia Arabia kuhusiana na mabadiliko ya ugavi wa nishati kwa mataifa ya Ulaya.

Wakati ambapo gesi ya Urusi inakosekana ama kutokana na vikwazo au kuzuwiliwa na Moscow, mataifa ya Ulaya yanahaha kutafuta vyanzo mbadala kwa nishati ya kuchimbwa ardhini.