1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bin Salman ziarani Ulaya

27 Julai 2022

Mrithi wa kiti cha ufalme cha Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, ameanza ziara yake ya Ulaya akitangaza miradi kadhaa, ukiwemo mkonga wa chini ya bahari utakaoipatia Ulaya "nishati jadidifu na ya bei rahisi."

https://p.dw.com/p/4EhrV
Greichenland Saudischer Kronprinz Mohammed bin Salman besucht Premieminster Kyriakos Mitsotakis
Picha: Costas Baltas/REUTERS

Mohammed bin Salman aliwasili mjini Athens jioni ya Jumanne (Julai 27), ikiwa ziara yake ya kwanza barani Ulaya tangu mauaji ya mwandishi wa habari wa Kisaudia, Jamal Khashoggi, yaliyofanyika kwenye ubalozi wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki, na ambayo uchunguzi wake ulimuweka yeye (Bin Salman) kwenye lawama za kuhusika moja kwa moja. 

Katika mkutano wake na waandishi wa habari akiwa na mwenyeji wake, Waziri Mkuu wa Ugiriki, Kyriakos Mitsotakis, mrithi huyo wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, alisema hii ni fursa ya kihistoria kwa pande zote.

Alisema anaamini wangelitumia fursa hii ya kihistoria kukamilisha makubaliano ya kuunganisha gridi ya umeme "utakoipatia Ugiriki na Ulaya ya Kusini Magharibi kupitia Ugiriki, nishati ambayo itakuwa rahisi zaidi na jadidifu pia."

Mrithi huyo wa kiti cha ufalme wa Saudia, alisema pia wangelishughulikia suala la haidrojini na jinsi ya kuigeuza Ugiriki kuwa kituo kikuu cha nishati hiyo kwa Ulaya.

Saudi Arabien | US-Präsident Biden trifft MSB
Rais Joe Biden akizungumza na Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia, Mohammed Bin Salman, tarehe 15 Julai 2022, mjini Jeddah, Saudi Arabia.Picha: Bandar Algaloud/Courtesy of Saudi Royal Court/Handout/AFP

"Hii ni fursa kubwa itakayobadilisha maisha yetu kwa sote." Aliwaambia waandishi wa habari.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Mitsotakis alithibitisha mpango huo, naye pia akisisitiza ni fursa ambayo italeta faida kubwa kwa pande zote mbili na hata eneo zima kwa ujumla wake. "Ni fursa ya kuthibitisha uimara wa mahusiano yetu ya kimkakati."

Mitsotakis alisema wangeliasaini muhimu na pia kujadiliana masuala ya kikanda na jinsi ya kuimarisha mahusiano baina ya Ugiriki na Saudi Arabia.

"Msisitizo mkubwa kwenye ushirikiano wa kiuchumi." Alisema waziri mkuu huyo wa Ugiriki.

Mauaji ya Khashoggi yamesahauliwa?

USA Washington Saudi-Arabien Journalist Jamal Khashoggi
Mchoro wa Jamal Khashoggi, mwandishi habari wa Kisaudia aliyeuawa mwezi Oktoba 2018 katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul, Uturuki, katika mauaji ambayo lawama zinaelekezwa kwa Mwana Mfalme wa Saudia, Mohammed Bin Salman.Picha: Yasin Ozturk/AA/picture alliance

Wachambuzi wa masuala ya kimataifa wanasema uhasama ulioongezeka baina ya Ulaya na Urusi kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, ambao unatishia Ulaya kukatiwa usafirishaji wa gesi wanayoitegemea sana kutoka Urusi, umewafanya viongozi wa Magharibi kujisahaulisha hasira walizokuwa nazo dhidi ya Bin Salman kufuatia mauaji ya Khashoggi ya mwaka 2018. 

Ulaya kwa sasa inahaha kutafuta njia za kujiondowa kwenye utegemezi wa nishati kutoka Urusi wakati huu vita vya Ukraine vikiendelea na majira ya baridi yakikaribia.

Ziara hii ya mwanamfalme huyo wa Saudi Arabia, ambaye kwa sasa ndiye kama mtawala halisi wa taifa hilo lenye utajiri wa mafuta, itamchukuwa hadi Ufaransa baadaye wiki hii, ambako atakutana na kufanya mazungumzo na Rais Emmanuel Macron.

Safari ya Bin Salman barani Ulaya inafanyika ikiwa wiki mbili tu baada ya Rais Joe Biden wa Marekani kuitembelea Saudia kwa mkutano wa kilele na viongozi wa Kiarabu, ambako alikutana ana kwa ana na Bin Salman.