1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano ya upinzani yaendelea kuiandama Kenya

13 Julai 2023

Maandamano ya kulalamikia ongezeko la gharama ya maisha yameendelea kuathiri sekta na hali mbali mbali nchini Kenya huku kukiwa na taarifa za vifo vilivyotokana na maandamano hayo.

https://p.dw.com/p/4Tr7y
Unruhen in Kenia
Picha: Luis Tato/AFP

Kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa na vyombo vya habari nchini humo, kufikia usiku wa Jumatano (Julai 12), watu tisa walikuwa wameshauawa na wengine 15 kujeruhiwa kwenye maandamano hayo. 

Shughuli za kibiashara zikiwemo usafiri na elimu ziliathirika katika maeneo mbalimbali hasa Nairobi, Mombasa, Kisumu, Migori, Nakuru, Homabay, Kisii, Nyamira na Machakos, ambako watu watatu waliripotiwa kufariki dunia. 

Kwenye maandamano hayo, maafisa wa polisi wawili walijeruhiwa.

Soma zaidi: Raila odinga apanga mikutano zaidi ya hadhara Kenya

Waandamanaji wameendelea kulalamikia gharama ya juu ya maisha, huku pia kukiripotiwa uvamizi wa makundi mengine ambayo yanapinga maandamano hayo kama ilivyoshuhudiwa jimbo la Kisii.

Hofu ya mapigano ya kikabila

Katika eneo la Sondu mpakani mwa majimbo ya Kisumu na Kericho, maandamano hayo yamezusha makabiliano kati ya jamii za eneo hilo ambazo zimekuwa na uhasama wa tangu jadi.

Unruhen in Kenia
Polisi wakiwakamata waandamanajiPicha: Luis Tato/AFP

Akizungumza na DW, mmoja wa wakaazi wa eneo hilo ambaye hakutaka jina lake kutajwa kwa sababu za kiusalama alisema "kufikia sasa watu watatu wamefariki kwenye ghasia hizo zilizochangiwa na maandamano ya jana."

Soma zaidi: Watu 6 wauawa katika maandamano ya upinzani Kenya

Kulingana na mwanamke huyo, wamelazimika kusalia majumbani mwao na kuwaondosha watoto shuleni wakati makabiliano ya makundi ya jamii za eneo hilo yakiendelea kushuhudiwa, licha ya juhudi za viongozi wa kisiasa eneo hilo kujaribu kutuliza hali.

Mashahidi wengine walisema makabiliano hayo baina ya makabila hasimu yalitumia mishale na kwamba katika watu waliouawa wamo waliofariki kwa mishale na risasi. DW haikuweza mara moja kuthibitisha madai hayo.

Ugoigoi wa vyombo vya usalama?

Kwenye ripoti kwa vyombo vya habari, gavana wa jimbo la Kisumu, Peter Anyang Nyong'o, alitoa wito kwa viongozi wa jimbo la Kericho kujitokeza kuzuia vurugu hizo za kijamii.

Unruhen in Kenia
Picha: Luis Tato/AFP

Nyong'o aliwakemea vikali maafisa wa polisi anaodai wamelegea kwenye kuwakabili wavamizi wanaovamia makaazi ya watu.

Soma zaidi: Polisi Kenya yatumia gesi ya machozi kutawanya waandamanaji

Katibu Mkuu wa chama cha ODM kinachounda muungano wa Azimio la Umoja, Edwin Sifuna, amenukuliwa katika vyombo vya habari nchini Kenya akisema ili kushinikiza serikali ya Rais William Ruto kuchukua hatua za kupunguza gharama ya maisha, wataendelea na maandamano hayo siku tatu mfululizo kuanzia Jumatatu.

Imetayarishwa na Musa Naviye/DW Kisumu