1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi Kenya yatumia gesi ya machozi kutawanya waandamanaji

12 Julai 2023

Polisi ya Kenya imefyetua mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji waliotikia wito wa kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, kuteremka mitaani na kupuuza marufuku iliyowekwa na vyombo vya usalama dhidi ya kuandamana

https://p.dw.com/p/4TlL2
Proteste in Kenia
Picha: Brian Inganga/AP/dpa

Katika mji mkuu, Nairobi, maduka mengi yalifungwa na usalama ulikuwa umemarishwa tangu mapema asubuhi kabla kutokea makabiliano baina ya polisi na wafuasi wa upinzani kwenye Mtaa wa Mathare wenye makaazi ya kipato cha chini.

Vurumai pia zimeshuhudiwa kwenye mji wa mwambao wa Mombasa ambako mabomu yalirushwa kuwakabili waandamanaji.

Maandamano ya leo ni mwendelezo wa yale yaliyofanywa wiki iliyopita na wafuasi wa upinzani wanaosema wanaipinga serikali kwa kushindwa kushughulikia kupanda kwa gharama za maisha na kuongeza kiwango cha kodi.

Maandamano hayo ya tarehe 7 Julai maarufu kama Saba Saba yaligeuka vurugu na kwa mujibu wa wizara ya mambo ya ndani watu 6 waliuwawa kwenye makabiliano yaliyotokea.