1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAfrika

Maambukizi ya covid-19 yapindukia 1,000 kwa siku Uganda

Lubega Emmanuel4 Juni 2021

Idadi ya wagonjwa wapya wa COVID-19 nchini Uganda imefikia watu 1,000. Hali hii imeleta hofu na mashaka kwa raia wa taifa hilo kufuatia kufurika kwa hospitali kwa wagonjwa mahututi na kwa hiyo mfumo wa afya kuzidiwa.

https://p.dw.com/p/3uQs0
Uganda I Impfstoff AstraZeneca
Picha: Badru Katumba/AFP/Getty Images

Msongamano wa magari ya kubeba wagonjwa kwenye hospiali kuu ya Mulago ni kielelezo tosha kuwa Uganda imo katika hatari kubwa ya janga la COVID-19.

Kulingana na wakuu katika wizara ya afya, hali hii imetokana na idadi kubwa ya watu kupuuza kanuni za kudhibiti ugonjwa huo hata baada ya aina za virusi kutoka Uingereza, Afrika Kusini, India na Nigeria kugunduliwa.

Soma pia: Covid-19 yatishia sekta ya elimu nchini Uganda

Kwa sasa hadi watu 1,000 kwa wastani wa kila siku wanagunduliwa kuwa na virusi hivyo. Daktari Ekwaru Obuku ambaye amekuwa akitoa ushauri kwenye mitandao ya kijamii kuhusu jinsi ya kujikinga dhidi ya COVID-19 na pia kujitibu mtu akipata dalili za awali za ugonjwa huo amesema hali ni mbaya.

Uganda I Impfstoff AstraZeneca
Muuguzi akiandaa dozi ya chanjo ya AstraZeneca katika hospitali kuu ya taifa ya Mulago nchini Uganda.Picha: Badru Katumba/AFP/Getty Images

Kampala kitovu cha maambukizi

Kwa mujibu wa takwimu za wizara ya afya na shirika la Afya duniani WHO, kiwango cha juu cha maambukizi kiko katika mji wa Kampala na viunga vyake.

Wimbi hili limeleta wasiwasi na baadhi ya vituo vya umma kama vile mahakama, shule na matawi ya benki vimefungwa kwa muda.Wafanyakazi wa afya wanaelezea kuzidiwa na shuguli za kuwahudumia wagonjwa mahututi wanaohitaji hewa ya oksijeni kwa dharura.

Soma pia: Janga la Covid-19 lazidisha ukiukwaji wa haki za binadamu

Rais Museveni anatarajiwa kutoa maelekezo mapya kuhusu njia za kudhibiti kasi hiyo ya maambukizi. Lakini baadhi ya wafanyabiashara hasa wa usafiri wa umma wanahofia kuwa huenda masharti makali ikiwemo kusitishwa kwa usafiri wa umma yatatangazwa.

Siku ya Alhamisi rais Museveni na mkewe walipata chanjo yao ya pili na kuwahimiza raia kwenda kupata chanjo hiyo ya bure. Wengi wameitikia mwito huo japo kuna baadhi ambao wangali wana mashaka kuhusu usalama wake.