1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani

Josephat Charo20 Juni 2005

Leo ni maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani. Wahanga kati ya milioni tisa na 25 wameelezwa kuwa wakimbizi wanaotafuta ufadhili katika mataifa yaliyoendelea ya magharibi ulimwenguni kote. Katika mataifa haya, wakimbizi wengi hukaribishwa, lakini hata hivyo sio wote wanaobahatika kukaribishwa. Mataifa ya magharibi huifunga milango yao huku mataifa maskini yanapowapokea wakimbizi wengi wanaohangaika. Je maadhimisho ya leo yatayaongeza matumaini ya wakimbizi duniani?

https://p.dw.com/p/CEFj
Wakimbizi wa eneo la Darfur nchini Sudan
Wakimbizi wa eneo la Darfur nchini SudanPicha: AP

Mkimbizi ni mtu ambaye amejaa hofu kwa yale yanayoendelea katika mazingira anamoishi, na anayeishi katika taifa la kigeni. Hofu hii inaweza kusababishwa na machafuko ya kisiasa ambayo hupelekea kuzuka kwa vita, hivyo ikawa watu wanakimbia kuyasalimisha maisha yao. Inawezekana pia ikawa mtu ni mfuasi wa dini ambayo haitakikani katika nchi yake, au akawa ni mwanachama wa kundi katika jamii au chama cha kisiasa kinachopinga serikali tawala. Mkimbizi huwa hana ulinzi wala usaidizi wa aina yoyote kutoka kwa serikali ya taifa lake, na hapo ndipo hulazimika kuihama nchi kutafuta mahala atakapoishi kwa amani na utulivu na kujisikia yu salama.

Maelezo haya yamo katika ibara ya kwanza ya sheria ya wakimbizi iliyotiwa saini mwaka wa 1951 mjini Genf. Kwa mujibu wa maelezo haya, inakadiriwa kwamba kuliwepo na wakimbizi milioni 9.2 mwaka jana. Tukiondoa maelezo yanayosema kwamba mkimbizi ni mtu anayeishi katika taifa la kigeni na tubakie na maelezo yale mengine, idadi ya wakimbizi duniani kote itaongezeka na kufikia kiwango kikubwa kisichoweza kumithilika.

Inakadiriwa kiwango hicho kinaweza kupindukia kati ya milioni 20 na 25 . Hii ni kwa maana kuna idadi kubwa ya watu ambao ni wakimbizi katika mataifa yao. Kunao wengi waliolazimika kuyahama makazi yao na wengine kuachwa bila makao kwa sababu ya yale yanayoendelea nchini mwao.

Ni mambo gani muhimu yanayofanywa na mataifa tajiri kukabiliana na tatizo la wakimbizi duniani? Kwa kweli sio mambo mengi. Mataifa mengi ya magharibi yanayothamini sana maongozi ya kidemokrasi, uhuru wa kujieleza, na kupigania haki za binadamu, yao yenyewe yamewafungia milangi wakimbizi wengi. Kwa mfano takwimu rasmi zinaonyesha kwamba Ujerumani imewakaribisha wakimbizi elfu 877 na Marekani kwa upande imewakubali wakimbizi elfu 421 pekee.

Ijapo Ujerumani inaweza kujivunia kwa kuwakaribisha wakimbizi wengi zaidi ikilinganishwa na Marekani, utayarifu wake wa kuwakaribisha wakimbizi bado haujayafikia mataifa maskini. Mataifa yanayoendelea ndiyo yanayobeba mzigo mkubwa zaidi likija swala la wakimbizi duniani. Iran inayashughulikia maslahi ya wakimbizi zaidi ya milioni moja kutoka Afghanistan, na Pakistan kwa upande wake imewakaribisha wakimbizi elfu 960. Katika eneo la Afrika Mashariki Tanzania imewaalika nyumbani wakimbizi zaidi ya milioni 600.

Mataifa tajiri yanatakiwa kuabika kwa takwimu hizi. Lakini yamelifungia macho tatizo hili, kana kwamba hakuna lolote linaloendelea. Jumuiya ya Ulaya kwa mfano imefanya juhudi za kuifunga mipaka yake. Mara kwa mara wakimbizi wengi kutoka Afrika wamekuwa wakijaribu kuingia Ulaya kwa njia ya madau kupitia baharini. Lakini mataifa ya Ulaya yamekuwa yakiwatia mbaroni na kuwahukumu kama wakimbizi wasio haramu. Wengi wao hufa maji baada ya madau yao kusombwa na mawimbi. Idadi kamili ya wale ambao wamefariki dunia baharini wakijaribu kuingia Ulaya bado haijulikani.

Mataifa tajiri yametoa sababu juu ya hatua ya kuwafungia milango wakimbizi. Yanasema yanawaruhusu wakimbizi ambao hawana fedha, wasio kazi wala bazi na ambao hawajifai kwa namna yoyote ile. Hiyo pengine ni sababu nzuri likizingatiwa swala la ongezeko la uhalifu unaosababishwa na baadhi ya wakimbizi hao. Hata hivyo, hata wale wakimbizi ambao wanasemekana ni halali, na wanaotafuta ufadhili katika mataifa hayo, wamesahaulika. Wakitaka kuwasalisha maombi ya kuruhusiwa kuishi katika taifa walilolifikia mwanzo kama wakimbizi, huambiwa haiwezekani. Ni lazima kufanya hivyo katika taifa lengine ambalo watapelekwa.

Idadi kubwa ya wakimbizi inapatikana barani Ulaya, hususan katikati mwa bara hili. Ni jambo la aibu kwamba misaada mingi ya fedha za kuwasaidia wakimbizi inatoka katika eneo hili lakini wakimbizi walio bahatika kufika mataifa tajiri bado wanatapatapa.

Wakati vyombo vya habari vinapotoa habari na kuonyesha picha za yale yanayoendelea katika eneo la Darfur nchini Sudan, ripoti hizo huchukuliwa na uzito mkubwa. Lakini jamii ya kimataifa haijitolei kikamilifu kuwasaidia wahanga wa Darfur. Shirika la wakimbizi la umoja wa mataifa liliripoti kwamba kati ya dola milioni 30 za kudhamini mradi wa kuwasaidia wakimbizi wa Darfur, ni milioni 1.5 pekee ambazo zimetolewa.

Maadhimisho ya leo hayatakuwa na maana yoyote ikiwa masilahi ya wakimbizi hayatashughulikwa kikamilifu kote duniani.