1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lukashenko hana dalili ya kuondoka madarakani huko Belarus

2 Septemba 2020

Nchini Belarus rais Alexander Lukashenko hana dalili ya kukaa pembeni licha ya shinikizo kuongezeka na kitisho cha vikwazo vya nchi za Magharibi. Marekani inafikiria kuwawekea vikwazo maafisa saba wa Belarus.

https://p.dw.com/p/3htlU
Belarus Präsident Lukaschenko
Picha: picture-alliance/AP Images/N. Petrov

Marekani imetangaza kupitia afisa wake mwandamizi katika wizara ya nje siku ya Jumanne kwamba wabelarus saba wanaoaminika walihusika katika udanganyifu wa matokeo ya uchaguzi pamoja na vurugu na kipigo dhidi ya watu waliokuwa wakifanya maandamano kwa amani ,watawekewa vikwazo.

Afisa huyo mwandamizi katika wizara ya nje ya Marekani ambaye amezungumza kwa sharti la kutotajwa jina amesema huenda Marekani ikafikiria vikwazo dhidi ya Urusi ikiwa nchi hiyo itaingilia mgogoro wa Belarus kwa kutumia nguvu.

Upinzani nchini Belarus unasema matokeo ya uchaguzi yalifanyiwa hila za udanganyifu ili kumpa nafasi rais Alexander Lukashenko aliyekaa madarakani miaka 26 aendelee kubakia kwenye nafasi hiyo.

Belarus Minsk Protest Demonstration
Maandamano ya upinzani mjini Minsk BelarusPicha: picture-alliance/AP Photo

Afisa huyo mwandamizi wa Marekani alikwenda mbali na kutowa maelezo ya ndani zaidi ya mazungumzo yaliyokwisha fanyika hadi sasa kati ya Naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani Stephen Biegun na maafisa wa Urusi huko mjini Moscow wiki iliyopita ambapo aliwaonya maafisa waandamizi wa Urusi dhidi ya kutumia nguvu nchini Belarus, ambayo iko katikati baina ya Urusi na nchi za Magharibi ,washirika wa jumuiya ya kujihami ya NATO.

Afisa huyo wa Marekani hakutaja majina ya maafisa hao saba wa Belarus watakaowekewa vikwazo lakini amesema rais Lukashenko tayari ameshawekewa vikwazo.Putin anaitaka Belarus inayoegemea upande wa Urusi

Wakati hayo yakiwekwa wazi kwa upande mwingine mpinzani mkuu nchini Belarus anayeyapinga matokeo ya uchaguzi wa rais Sviatlana Tsikhanouskaya, anatarajiwa siku ya ijumaa kuzungumza mbele ya mkutano usio rasmi wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Lithauen Vilnius | Sviatlana Tsikhanouskaya
Aliyekuwa mgombea wa upinzani wa Belarus Sviatlana TsikhanouskayaPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Kulbis

Balozi wa Estonia katika Umoja huo wa Mataifa Sven Jurgenson amesema mgombea huyo wa urais wa upinzani nchini Belarus aliyekimbilia Lithuania kufuatia shinikizo la maafisa wa Belarus atazungumza katika kikao hicho hasa kuhusu kushambuliwa kwa haki za binadamu katika nchi hiyo iliyokuwa chini ya Umoja wa kisovieti.

Maelezo ya afisa mwandamizi wa Marekani kuhusu hatua inayopangwa kuchukuliwa na nchini yake inakuja baada ya wiki iliyopita rais wa Urusi Vladmir Putin kusikika akisema kwamba alishaweka jeshi la polisi la akiba la kwenda kumuunga mkono rais Lukashenko ikiwa itahitajika ingawa bado hajaona haja ya kulipeleka jeshi hilo kwa sasa.

Ikumbukwe kwamba Belarus bado inauhusiana wa karibu sana wa kisiasa kiuchumi na kitamaduni na Urusi na ni mwanachama wa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Urusi. Nchi hizo mbili pia zimeunganishwa na mkataba wakimaandishi unatangaza muungano wa dola,ambao rais Putin ameamua kuupa nguvu na kuupeleka katika hatua nyingine zaidi ya kisiasa na kiuchumi.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW