Putin anaitaka Belarus inayoegemea upande wa Urusi
21 Agosti 2020Uamuzi wa Umoja wa Ulaya wa kukataa kumtabua Alexander Lukashenko kama kiongozi halali wa Belarus, umesababisha kiongozi huyo kufanya chochote anachokitaka kwani haoni tena haja ya kuuthamini umoja huo wenye makao yake mjini Brussels, Ubelgiji.
Katika mkutano na baraza lake la ulinzi, Lukashenko aliaamrisha polisi kutumia nguvu kuzima maandamano ya kupinga serikali katika mji mkuu Minsk, maandamano ambayo mwenyewe ameyataja kuwa ni “vurugu na usumbufu”
Kidole cha lawama dhidi ya mataifa ya kigeni
Kwa kiasi fulani kama ilivyotabiriwa kiongozi huyo pia aliyeelekeza kidole cha lawama kwa mataifa ya kigeni na kuyatuhumu kwa kile alichosema kuchochea maandamano ya kuipinga serikali yake huku akiaamrisha wanadiplomasia wake “kutoa onyo kwa viongozi wa Magharibi” akiwemo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, kuwa atawawaajibisha kwa kuingilia kati katika mambo ya ndani ya Belarus.
Huenda sababu ya Lukashenko kutoa matamshi hayo yenye kuonyesha nguvu na kujiamni ni kutokana jawabu katika mawasiliano baina yake na rais wa Urusi Vladmir Putin. Katika siku za hivi karibuni, viongozi hao wawili wameshiriki mazungumzo mara nne kupitia njia ya simu.
Licha ya kutokuwepo na muelewano mzuri kati ya Putin na Lukashenko, kwa sasa ni dhahir kwamba mshirika wa karibu wa uongozi wa kisiasa wa Minsk ni Urusi na rais Putin atafanya juu chini ili kumwezesha mwenzake Lukashenko kusalia madarakani hata kama itahitaji kuingilia kati kijeshi.
Kuanzia kuingilia kati kijeshi nchini Syria ili kumsaaidia Bashar al-Assad kuendeela kushika usukani hadi kumuuunga mkono Rais Nicolas Maduro wa Venezuela Putin anajitizama kama kiongozi bingwa mwenye kuokoa utawala wa kiimla ambao unakuwa matatani.
Zaidi ya hayo kwa mtizamo wa rais huyo, Belarus ni nchi ambayo umuhimu wake hauwezi kulinganishwa na mataifa mengine ambayo amekuwa akiingilia. Mbali na kusaini mikataba kadha kati nchi hizo mbili, uchumi wa Belarus kwa kiasi kikubwa unaitegemea Urusi. Mataifa hayo mawili pia yana mfumo moja wa kudhibiti mipaka yake pamoja na mfumo wa pamoja wa ulinzi dhidi ya mashambuzi ya angani.
Mwandishi Konstantin Eggert anasema kwamba ikiwa vuguvugu la maandamano litamng’oa madarakani Lukashenko, itakuwa pigo kubwa kwa Putin na huenda akapoteza sifa. Kulingana na mwandishi huyo vuguvugu la waandamanaji wenye wazo la “nguvu ya watu’’ ambao wana imani kwamba raia wa kawaida wanaweza kubadilisha utawala ni moto wa kuotea mbali kwa rais Putin.
Rais huyo anahofu kuwa huenda raia nchini mwake wakatumia njia hiyo hiyo na kuandamana dhidi ya utawala wake wa kiimla na kuyapatia mwanya mataifa ya Magharibi kumuondosha mamlakani.
Lukashenko kulipia gharama ya msaada wa Kremlin
Kwa sasa ikulu ya Urusi Kremlin itajizuiwa na hatua ya kutuma wanajeshi wake nchini Belarus kumsaidia Lukashenko, hata hivyo ni mapema kuthibitisha kuwa hakuna uwezekano wa kufanya hivyo kabisa. Iwapo Lukashenko atanusurika kuondolewa madarakani kwa usaidizi wa Urusi, rais huyo huenda akalipia gharama ya usaidizi wa Urusi kwa kuridhia matakwa ya Moscow kama kutambua, unyakuzi wa Urusi wa eneo la Crimea pamoja na kuikubali Urusi kuanzisha kambi za kijeshi nchini humo.
Kwa upande mwingine, ikiwa atalazimika kuondoka ofisini, Putin huenda akatumia njia mbadala. Katika uchaguzi mpya, ikulu ya Kremlin bila shaka itamuunga mkono mgombea mwenye kuelemea Urusi bila kujali atakuwa nani.
Hofu kubwa kwa rais huyo ni kuiona Belarus yenye utawala wa Kidemokrasia ambao unaelemea Magharibi na wenye sera rafiki kwa Umoja wa Ulaya. Katika wakati huu ni vigumu kufikiria kwamba huenda hilo linaweza kutokea, lakini Putin hangependa kuthubutu na anajaribu kuzuia hali kama hiyo.