1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

London. Blair aiita imani kali ya Uislamu kuwa ni nadharia ya kishetani.

17 Julai 2005
https://p.dw.com/p/CEts

Waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair ameiita imani kali ya Uislamu kuwa ni nadharia ya kishetani. Akizungumza mjini London , Blair alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kupambana na kuondoa fikira hizo kutoka kwa watu wenye imani ya nadharia hizo.

Waziri mkuu huyo ametoa matamshi hayo wakati akizungumzia mashambulio ya wiki iliyopita dhidi ya mji wa London, ambayo yalisababisha vifo vya watu 55 na kuwajeruhi watu wengine zaidi ya 700.

Polisi wametoa picha za video za watu hao wanne wanaotuhumiwa kulipua mabomu hayo. Watatu kati ya watu hao wanne wametembelea Pakistan hivi karibuni na majeshi ya usalama nchini Pakistan yanasema kuwa wamewakamata watu wanane kwa kuhusika na mashambulio hayo ya mabomu.

Wakati huo huo , nchini Misr, polisi wanamhoji mwanakemia anayesoma nchini Uingereza kwa tuhuma za kuhusika na mashambulio hayo. Lakini waziri wa mambo ya ndani nchini Misr amesema katika mahojiano na gazeti moja kuwa mtu huyo hana uhusiano na mtandao wa kigaidi wa al Qaeda.