1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leo ni maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Demokrasia

15 Septemba 2022

Septemba 15 dunia inaadhimisha siku ya Kimataifa ya Demokrasia. Siku hii ilianzishwa kupitia azimio lililopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 2007, likihimiza serikali duniani kuimarisha demokrasia.

https://p.dw.com/p/4Gszz
Türkei | Besuch Antonio Guterres in Istanbul
Picha: Khalil Hamra/AP Photo/picture alliance

Mwaka huu, siku ya kimataifa ya Demokrasia imejikita katika kuzingatia umuhimu wa vyombo vya habari katika kukuza demokrasia, amani na kutimiza malengo ya maendeleo endelevu.

Vyombo vya habari vilivyo huru vinatajwa kuwa viungo muhimu vya kuuelimisha umma kuhusu masuala yanayowagusa moja kwa moja, swala ambalo ni muhimu katika kukuza demokrasia.

Kupitia mchango wa vyombo vya habari, umma unapata nafasi ya kufanya maamuzi sahihi na kuiwajibisha serikali. Hata hivyo, kuna madhara makubwa hasa wakati vyombo vya habari vinapobinywa.

Soma pia: CPJ yaitaka DRC kuwaachia huru wanahabari walio kizuizini

Licha ya miito ya kuvitaka vyombo vya habari kutekeleza majukumu yao pasi na kuingiliwa, waandishi wa habari duniani kote wanakabiliwa na vikwazo vya kuwawezesha kufanya kazi zao kwa uhuru- na athari yake huonekana kwa kutoheshimiwa kwa haki za binadamu, demokrasia na maendeleo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake kwa njia ya video wakati wa kuadhimisha siku ya kimataifa ya demokrasia, ametilia mkazo umuhimu wa vyombo vya Habari.

Amesema ulimwengu hauwezi kuendelea bila kuwepo uhuru wa vyombo vya Habari na uhuru wa kujieleza, "Leo ni maadhimisho ya miaka 15 ya siku ya kimataifa ya demokrasia, lakini kote ulimwenguni demokrasia inarudi nyuma. Raia hawashirikishwi, kutoaminiana na taarifa potofu zinaongezeka. Taasisi za kidemokrasia zinadhoofishwa. Sasa ni wakati wa kuzungumza. Sasa ni wakati wa kusimama na demokrasia,  maendeleo na kutetea haki za binadamu. Vyote hivyo vinategemeana na vinahitaji kuimarishwa."

Waandishi wa habari wanawake wanatajwa kuwa hatarini zaidi.

Symbolbild Pressefreiheit
ICFJ imesema waandishi wa habari wanawake wameripoti kukumbana na visa vya unyanyasaji wakati wanapofanya kazi zao.Picha: Christoph Soeder/dpa/picture alliance

Katika kuadhimisha siku hii ya kimataifa ya demokrasia mwaka huu, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya ushirikiano inaanda majadiliano juu ya umuhimu wa kulinda uhuru wa vyombo vya habari kama sehemu ya kukuza demokrasia imara.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni UNESCO limeripoti kuwa asilimia 85 ya watu duniani wameshuhudia kupungua kwa uhuru wa vyombo vya habari nchini mwao katika kipindi cha miaka mitano.

Soma pia: RSF:Ujerumani imeporomoka kwa uhuru wa habari

Vyombo vya habari katika sehemu mbalimbali duniani vinashambuliwa, waandishi wanakamatwa kiholela na kuwekwa kizuizini, mamlaka kutumia sheria kandamizi ili kubinya uhuru wa kujieleza pamoja na mbinu nyengine- dhamira kuu ya hayo yote ni kuzuia kazi za waandishi wa habari.

Kadhalika, janga la ugonjwa wa UVIKO-19 pia limeonyesha umuhimu wa vyombo vya habari kukusanya na kutathmini uhalisia wa ripoti zinazochapishwa mtandaoni, maana kumechapishwa ripoti potofu chungunzima kuhusu ugonjwa huo.

Waandishi wa habari wanawake wanatajwa kuwa ndio wako hatarini zaidi.

UNESCO na shirika la kimataifa la waandishi ICFJ imegundua kuwa asilimia 73 ya waandishi wa habari wanawake 714 katika jumla ya nchi 125 wameripoti kukumbana na visa vya unyanyasaji mitandaoni wakati wa kazi zao.

Aidha kuna juhudi za makusudi zinazofanywa ili kuwafunga midomo waandishi wa Habari, na wakati mwengine hata hupoteza maisha yao.

Kuanzia mwaka 2016 hadi mwishoni mwa mwaka 2021, UNESCO imerekodi mauaji 455 ya waandishi wa habari, ambao aidha walikufa kutokana na kazi zao au wengine waliuawa wakiwa wanatekeleza majukumu yao ya kupasha umma habari.