1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

''Lazima tukope '' asema Rais Samia

Florence Majani4 Januari 2022

Rais Samia Suluhu ameweka wazi kutokuridhishwa kwake na makundi yanayoukodolea jicho urais kwenye uchaguzi wa mwaka 2025, huku akisisitiza msimamo wake wa kuendelea kupopa.

https://p.dw.com/p/458XN
Tansania l Neue Präsidentin Samia Suluhu Hassan
Picha: AP/picture alliance

Akitumia muda mrefu kuzungumzia tafauti yake na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai, Rais Samia aliigeuza hafla ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa matumizi ya fedha za maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya Covid-19, kuwa jukwaa la kumjibu mkuu huyo wa muhimili wa chombo cha kutunga sheria. Rais Samia amesema aliwahi kuelezwa na mzee mmoja kuwa angelisumbuliwa na mwenye shati la kijani mwenzie anayetazama 2025 na sio mpinzani. Akasisitiza kuwa yanayoendelea ni msongo wa 2025.

''... Atakaye kusumbua kwenye kazi yako na uongozi wako ni shati ya kijani mwenzio wala si mpinzani. Huyo ndio atakaye kusumbua,anayetizama mbele mwaka 2025 na 2030 huyo ndiye atakaye kusumbua'',alisema Samia akizungumzia ujumbe alioletewa,alipochukuwa madaraka.

Soma piaRais Samia asema yuko tayari kuvumilia na kusamehe

''Tutaendelea kutozana tozo''

Spika wa bunge la Tanzania Job Ndugai
Spika wa bunge la Tanzania Job NdugaiPicha: DW/H. Bihoga

Kuhusu mikopo Rais amesema ili kuleta ustawi wa nchi ni lazima utumie kila njia ili kuhakikisha taifa lina maendeleo hivyo akasisitiza kuwa tozo zinaendelea na kama ni kukopa kunasaidia basi Tanzania itaendelea kukopa. Akaongeza hata kama mikopo inawachefua watu lakini itaendelea kukopa na sio kioja kwani si mara ya kwanza Tanzania inakopa. 

''Kwa hiyo kama kuna tozo ,tutaendelea kutozana tozo,na sisi sio wa awalai kwenye tozo. Nchi nchungu nzima wanamatozo makubwa kuliko ya kwetu. Hata hao walioendelea. kwa hiyo tutaendelea.'',alisema Samia.

Soma pia: Job Ndugai amuomba radhi rais Samia na Watanzania

Je, CCM kuelekea mpasuko ?

Wafuasi wa chama tawala CCM
Wafuasi wa chama tawala CCMPicha: AP

Rais Samia amesema fedha za mikopo zinakwenda kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwamo afya, miundombinu, umeme na akasisitiza kuwa umeme si anasa bali ni lazima.

Kadhalika Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba amesema Tanzania imepata mkopo usio na riba wa Tsh 1.3 trilioni na akaongeza kuwa mikopo sio msaada bali anapewa mwenye chanzo cha kulipa.Mwigulu amesema tathimini ya uhimilivu wa deni uliofanyika Novemba unaonyesha deni la nchi ni himilivu kwa kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.

Katika hafla hiyo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mawaziri wengine walifafanua na kufanya tathmini ya miradi ya maendeleo iliyofanywa katika kipindi kifupi cha Rais Samia kuwa madarakani. Miradi hiyo ni pamoja na elimu, barabara, maji, umeme na afya.