1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kundi lenye silaha lataka uzalishaji mafuta kusitishwa Libya

John Juma Mhariri: Daniel Gakuba
9 Juni 2020

Shirika la taifa la mafuta la Libya (NOC) limesema leo kuwa kikosi kilichojihami kwa silaha kiliingia katika eneo lake la Shahara lenye visima vya mafuta, na kuwaamuru wafanyakazi wake kulifunga eneo hilo.

https://p.dw.com/p/3dUc9
Libyen, Tripoli: Übernahme des Flughafens
Picha: picture-alliance/H. Turkia

Tukio hilo limejiri saa kadhaa baada ya shirika hilo kurejelea operesheni zake.

Shirika hilo la mafuta la Libya (NOC) limeongeza kwenye taarifa yake kwamba limewaambia wafanyakazi wake kutoiheshimu amri hiyo ya kusitisha operesheni zake katika eneo hilo la visima vya mafuta. Hata hivyo taarifa hiyo haikueleza waziwazi ni kikosi kipi haswa chenye silaha kilitoa amri hiyo.

Mnamo siku ya Ijumaa, walinzi wa vituo hivyo vya mafuta walisema kuwa bomba linalopeleka mafuta Hamada kutoka visima vya Shahara lilifunguliwa baada ya kufungwa kutokana na marufuku ya uuzaji wa mafuta na bidhaa nyinginezo za mafuta.

Katika tukio jingine, ofisi ya rais wa Uturuki imesema Rais Recep Tayyip Erdogan pamoja na rais wa Marekani Donald Trump wamefanya mazungumzo kwa njia ya simu na kukubaliana kuimarisha ushirikiano wao kuhusu Libya.

Trump na Erdogan kushirikiana kuhusu Libya

Ofisi hiyo imeongeza kuwa makubaliano kati ya Trump na Erdogan yanalenga kuimarisha amani na uthabiti wa Libya.

Libya ni taifa lenye utajiri mkubwa wa mafuta. Hii ni mojawapo ya visima vyake vya mafuta karibu na Murzuq.
Libya ni taifa lenye utajiri mkubwa wa mafuta. Hii ni mojawapo ya visima vyake vya mafuta karibu na Murzuq.Picha: Reuters/A. Lewis

Uturuki inaiunga mkono serikali ya kitaifa ya Libya (GNA) inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa, na imeimarisha msaada wake wa kijeshi kwa serikali hiyo, katika vita vyake dhidi ya mbabe wa kivita Khalifa Haftar anayeviongoza vikosi vyake vilivyoko mashariki mwa nchi hiyo.

Kwa upande mwingine, ni rasmi kuwa Marekani inaunga mkono serikali ya Libya GNA. Lakini Haftar anaungwa mkono na washirika wa Marekani kama vile Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na Saudi Arabia.

Pigo kwa vikosi vya Haftar

Uturuki imeisadia GNA kwa kuipa ndege zisizohitaji marubani yaani drones pamoja na mifumo ya ulinzi dhidi ya mashambulizi ya angani. Misaada ambayo katika wiki za hivi karibuni, imevisaidia vikosi vyake kufanya misururu ya mashambulizi na kuulemea upande wa Haftar.

Shirika la mafuta la Libya NOC, limedai kuwa hatua ya vikosi vya Haftar kupiga marufuku uuzaji w amafuta kutoka katika maeneo yanayodhibiti yanatishia viwango vya uzalishaji mafuta nchini humo.
Shirika la mafuta la Libya NOC, limedai kuwa hatua ya vikosi vya Haftar kupiga marufuku uuzaji w amafuta kutoka katika maeneo yanayodhibiti yanatishia viwango vya uzalishaji mafuta nchini humo.Picha: picture-alliance/AP Photo/H. Malla

Haftar na vikosi vyake wamekuwa wakipambana kuchukua udhibiti wa mji mkuu Tripoli.

Nayo serikali ya Ujerumani imesema Kansela Angela Merkel amezungumza na rais wa Misri Abdel Fattah al-Sissi kuhusu hali ilivyo Libya, na kwamba Merkel amesema mazungumzo yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa yanasalia kuwa lengo kuu la kuleta amani ya kudumu Libya.

Mnamo siku ya Jumamosi, Rais al-Sissi alipendekeza usitishaji vita baada ya vikosi vya GNA na washirika wake kushambulia na kuchukua udhibiti wa maeneo kadhaa yaliyokuwa yakidhibitiwa na vikosi vya Haftar, na hivyo kuhitimisha juhudi za Haftar kuliunganisha taifa hilo kwa nguvu na kwa ushirikiano wa Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu na Urusi.

Vyanzo: RTRE, AFPE