1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zogo yaendelea kuigubika Libya

Saumu Mwasimba Mhariri: Mohamed Khelef
28 Aprili 2020

Serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa nchini Libya imemtuhumu mpinzani wake mkuu, kiongozi wa kijeshi mwenye usemi, Khalifa Khaftar, kwamba anataka kuanzisha mapinduzi mengine.

https://p.dw.com/p/3bWQr
Fernsehansprache: Chalifa Haftar
Picha: Reuters TV

Khalifa Khaftar amedai kwamba amepata kibali cha wananchi kuiongoza nchi hiyo ya Afrika Kaskazini.

Mjini Tripoli ndiko iliko serikali ya Libya inayotambuliwa kimataifa ambayo imetowa taarifa kabla ya alfajiri ya Jumanne ikisema kamanda huyo wa kijeshi mwenye nguvu kubwa zaidi upande wa mashariki mwa nchi hiyo, ameanzisha operesheni nyingine mpya za kufanya mapinduzi kutwaa uongozi wa taifa hilo.

Kamanda huyo wa kijeshi, Khalifa Khaftar, anayelidhibiti kikamili eneo kubwa la mashariki mwa nchi hiyo na aliyeanzisha operesheni kubwa mwezi Aprili mwaka jana ya kuutwaa mji mkuu, Tripoli, alisema jana Jumatatu kwamba jeshi lake limeridhia matakwa ya wananchi wa Libya na kibali ilichowapa kuiongoza nchi hiyo.

Lakini kamanda huyo hakuweka wazi ikiwa bunge lililochaguliwa mwaka 2014 na ambalo pia lipo mashariki linaiunga mkono hatua yake.

Kimsingi Haftar anadai uhalali wake umetokana na bunge hilo lilolazimika kuhamishia makao yake makuu mashariki baada ya mji wa Tripoli kusambaratishwa na vita miaka sita iliyopita.

Mnamo Jmatatu, alitangaza kwamba makubaliano ya mwaka 2015 yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa na kuzaa serikali ya Umoja wa kitaifa iliyoko Tripoli yamekufa.

Juhudi za kuleta amani Libya bado hazijafua dafu.
Juhudi za kuleta amani Libya bado hazijafua dafu.Picha: Imao-Images/Xinhua/A. Salahuddien

Tangazo hili limezidi kuyavuruga mambo na kuondowa kabisa matumaini ya kupatikana suluhisho la kisiasa katika mgogoro huo wa kuwania madaraka Libya.

Marekani imetowa mwito wa kufanyika mazungumzo kati ya pande hizo mbili na kufikia makubaliano ya kusitisha vita kwa msingi wa kibindadamu.

Lakini pia Marekani imesikitishwa na msimamo huo wa Haftar ikisema ni azimio la mtu mmoja linalobadili mpagilio mzima wa kisiasa nchini Libya. Wanajeshi wa Haftar kwa upande mwingine wanadai wapinzani wao mjini Tripoli wameanzisha mashambulizi dhidi yao baada ya ndege isiyokuwa na rubani ya Uturuki kuushambulia msafara wa malori ya chakula huko upande wa magharibi mwa Libya na watu wasiopungua watano kuuwawa. Makundi yanayoisadia serikali hiyo dhaifu ya Tripoli yamekanusha kuhusika.

Ikumbukwe kwamba wanaompinga Khalifa Haftar wanamtuhumu kuwa ni mtu kwa namna zote anayetaka kuleta udikteta mpya wa kijeshi nchini Libya. Hii sio mara ya kwanza kwa mbabe huyo wa kivita kuyauwa makubaliano ya mwaka 2015 yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa. Alifanya hivyo mwaka 2017 na miaka mitatu kabla ya hapo aliwahi kutangaza kupitia televisheni kwamba amechukuwa madaraka ya kuiongoza Libya.

Mamia ya Walibya wameshauwawa tangu Haftar alipoanzisha operesheni yake ya kutaka kuudhibiti mji mkuu Tripoli na kiasi wengine 200,000 wamepoteza makaazi yao.

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW