1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al-Shabab yadai kuhusika na shambulio la jijini Mogadishu.

10 Juni 2023

Kundi la kigaidi la Al-Shabab limedai kuhusika na shambulio kwenye hoteli moja maarufu katika mjini Mogadishu siku ya Ijumaa.

https://p.dw.com/p/4SPrP
Somalia Militants Twitter
Picha: picture alliance / AP Photo

Kundi la kigaidi la Al-Shabab limedai kuhusika na shambulio kwenye hoteli moja maarufu katika mji mkuu Mogadishu jana Ijumaa ambalo limesababisha majeruhi ya takriban watu saba.

Shirika la habari la serikali limeandika kwenye mtandao wao wa Twitter kuwa vikosi vya usalama vinaendesha oparesheni ya kuwasaka wapiganaji wa Al-Shabab waliohusika na shambulio hilo.

Shirika hilo limeripoti kuwa, "raia wengi" wameokolewa wakiwa hai kutoka hoteli hiyo ya Pearl huku mapigano yakiendelea usiku kucha. Hakuna ripoti zozote za vifo vilivyotokea kutokana na shambulio hilo.

Shambulio katika hoteli ya Pearl ilioko ufukweni mwa bahari lilitokea mapema jana jioni.

Mkurugenzi wa kampuni ya Amin inayomiliki magari ya kubebea wagonjwa Abdikadir Abdirahman amesema wamepokea watu saba waliojeruhiwa katika shambulio hilo.

Kundi la Al-Shabab lenye mafungamano na mtandao wa Al-Qaeda limesema katika taarifa kuwa, wapiganaji wake wamefanikiwa kuingia katika hoteli ya Pearl ilioko ufuoni mwa bahari na kwamba bado wanaudhibiti.

Kundi la Al-Shabab lenye makao yake nchini Somalia linajulikana kwa kufany mashambulizi kwenye hoteli za kifahari na maeneo yenye kutembelewa na watu mashuhuri mjini Mogadishu, aghalabu huanza kwa kufanya shambulio la bomu la kujitoa mhanga.

Hoteli ya Pearl iko karibu na ubalozi wa Uturuki na hutembelewa sana na viongozi na maafisa wakuu wa serikali ya Mogadishu.