1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kumbukumbu za shambulizi dhidi ya waumini wa Kiyahudi Halle

9 Oktoba 2020

Wakaazi wa mji wa Halle ulio mashariki mwa Ujerumani wanawakumbuka wale waliouwawa katika shambulio dhidi ya waumini wa Kiyahudi kwenye sinagogi moja mjini humo.

https://p.dw.com/p/3jhC3
Halle | Gedenken an Anschlag auf Synagoge |
Picha: Hendrik Schmidt/dpa/picture alliance

Licha ya mshikamano uliopo baada ya shambulio hilo, wengi katika jamii ya Kiyahudi wanahisi serikali haikuchukua hatua za kutosha kulikabili suala hilo. 

Max Privorozki ni mmoja kati ya watu 52 waliokuwa wanasherehekea sikukuu ya Yom Kippur, moja ya siku takatifu kabisa katika kalenda ya Mayahudi ndani ya sinagogi moja mjini Halle mnamo Oktoba 9 mwaka 2019, wakati kijana wa miaka 27 kutoka mji jirani alipojaribu kuingia kwa nguvu ndani ya sinagogi hilo akiwa amejihami kwa bunduki pamoja na mabomu.
Soma pia: Mshambuliaji wa sinagogi Halle apandishwa kizimbani

Mshambuliaji huyo alishindwa kwa kiasi kikubwa kuingia katika jengo hilo kufuatia ulinzi mkali uliokuwepo katika eneo hilo. Mlango imara pamoja na kamera za CCTV zilizuwiya shambulio ambalo lingelikuwa shambulio baya zaidi dhidi ya jamii ya Mayahudi nchini Ujerumani tangu kumalizika kwa mauaji ya Holocaust wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.

Hata hivyo, polisi wa Ujerumani hawakuonekana majasiri katika kukabiliana na shambulio hilo katika mji huo wa mashariki mwa Ujerumani. Max Privorozki, kiongozi wa jamii ya wayahudi alikiambia chombo cha habari cha MDR kwamba na hapa ninamnukuu "Tumesema mara kadhaa kwamba tunahitaji ulinzi wa polisi mbele ya majengo ya sinagogi na jamii katika jimbo la Saxony-Anhalt ambako mji wa Halle uko chini yake, kama ilivyo mjini Berlin, Munich na Frankfurt. Lakini mara zote tunaambiwa kila kitu kiko sawa." Mwisho wa kumnukuu.

Wengi katika jamii ya Kiyahudi wanahisi serikali haikuchukua hatua za kutosha kulikabili suala hilo. 
Wengi katika jamii ya Kiyahudi wanahisi serikali haikuchukua hatua za kutosha kulikabili suala hilo. Picha: Hendrik Schmidt/dpa/picture alliance

Soma pia: Merkel ataka chuki dhidi ya Wayahudi ikabiliwe

Kwa sasa imebainika kufuatia kesi inayoendelea mahakamani, polisi walishindwa kumgundua mshambuliaji aliyeendesha gari akitoka katika sinagogi hilo baada ya shambulio baada ya kuwauawa watu wawili ambao sio kutoka jamii ya Kiyahudi.

Kwa upande wake, Rais wa Baraza la Mayahudi nchini Ujerumani, Josef Schuster, amesema uzembe wa serikali haukuweza kuvumiliwa.

Tangu wakati huo, polisi katika eneo hilo imejaribu kusuluhisha mambo kwa kujenga tena uaminifu kati yao na jamii hiyo, na kwa sasa wapo katika mawasiliano ya karibu na jamii ya Mayahudi mjini Halle kuhusu masuala ya usalama.

Upande wa kisiasa nao pia haujasaidia vya kutosha katika suala hili. Mapema wiki hii, waziri wa ndani wa jimbo la Saxony-Anhalt, Holger Stahlknecht, alizua gumzo kwa kusema kuwa moja ya wajibu mpya wa kuilinda jamii ya Mayahudi inamaanisha kuwa polisi hawatofika kwa haraka kushughulikia masuala mengine.

Hata hivyo, Josef Schuster amekanusha vikali hilo akisema waziri wa ndani, Holger Stahlknecht, amekosa haya kuwatambulisha Mayahudi kama jamii inayopendelewa au kupewa kipaumbele kuliko makundi mengine. Amesema tamko alilolitoa Stahlknecht, linaendeleza chuki dhidi ya Mayahudi.

Rais wa Baraza la Mayahudi nchini Ujerumani, Josef Schuster.
Rais wa Baraza la Mayahudi nchini Ujerumani, Josef Schuster.Picha: Hendrik Schmidt/dpa/picture alliance