1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongo yachagua rais katikati mwa hofu ya udanganyifu

20 Desemba 2023

Kongo inafanya uchaguzi wa rais, wabunge, magavana na wawakilishi wa manispaa, katikati mwa changamoto kubwa za lojistiki na usalama, huku upigaji kura ukichelewa kwa takribani masaa mawili na nusu mjini Kinshasa.

https://p.dw.com/p/4aOzX
DR Kongo | Uchaguzi wa Rais 2023 | Kituo cha kura Goma
Mwanamke akitekeleza haki yake ya kupiga kura mjini Goma, Desemba 20, 2023.Picha: Arlette Bashizi/REUTERS

Takribani watu milioni 44,  karibu nusu ya idadi ya wakazi wote, walitarajiwa kupiga kura, lakini wengi, ikiwa ni pamoja na milioni kadhaa waliokimbia makazi yao kutokana na vita katika eneo kubwa la mashariki mwa nchi hiyo, wanaweza kuhangaika kupiga kura zao. Mapigano hayo yamewazuia watu milioni 1.5 kujiandikisha kupiga kura.

Kilichoko hatarini ni uaminifu wa kura hiyo katika mojawapo ya mataifa makubwa zaidi barani Afrika na ambayo rasilimali zake za madini zinazidi kuwa muhimu kwa uchumi wa dunia.

Kongo ina historia ya uchaguzi wenye utata ambao unaweza kugeuka kuwa wa vurugu na tayari kuna mzozo mkubwa wa imani kwa taasisi za nchi hiyo. Wachambuzi wanasema matokeo yoyote ya kutiliwa shaka hayawezi tu kuiingiza nchi katika machafuko bali inaweza kuwa na athari katika eneo ambalo lina historia ya mapinduzi ya kijeshi.

"Katika nyakati za mapinduzi na udikteta barani Afrika, uchaguzi huu ni fursa ya kuimarisha demokrasia ya kipekee katika Afrika ya kati," alisema Fred Bauma, mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya utafiti ya Kongo ya Ebuteli.

DR Kongo | Uchaguzi wa Rais 2023 | Kituo cha kura Kinshasa
Wapigakura wakihakiki majina yao kwenye orodha ya wapigakura mjini Kinshasa, Desemba 20, 2023.Picha: John Wessels/AFP/Getty Images

Siku ya Jumatano wapiga kura walijipanga kwa saa kadhaa wakisubiri kupiga kura zao. "Unapoamka asubuhi unatazamia mambo mazuri, kazi nzuri, na mimi nataka usalama," alisema Raymond Yuma katika mji mkuu, Kinshasa. Alikuwa amekaa kando ya watu wengine watatu kwenye benchi akingoja kwenye foleni ili milango ifunguliwe. Wote kadi zao za kupigia kura zilikuwa hazisomeki.

Soma pia; Raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wapiga kura leo

Katika eneo la Mashariki mwa Kongo, watu walisema walikuwa hawapati majina yao kwenye orodha za kura. "Wapiga kura walioonyeshwa kwenye orodha katika vituo vya kupigia kura ni wachache kuliko waliojipanga. Sipati jina langu kwenye orodha na hii inaweza kusababisha misukosuko hapa kwa sababu pia nataka kupiga kura," alisema Jules Kambale kwenye kituo cha kupigia kura mjini Goma.

Changamoto za usambazaji, vitambulisho

Wakingoja upigaji kura kufunguliwa wakati wa kucheleweshwa kwa zaidi ya saa mbili, watu walikua na wasiwasi na kuanza kubishana, haswa katika mji mkuu. Hata baada ya vituo kufunguliwa, wengi walikatishwa tamaa na mchakato huo wa polepole. Katika kituo kimoja cha kupigia kura, umati wa watu wenye hasira ulijaribu kuwapita maafisa wa polisi waliokuwa wakilinda lango la kituo hicho.

Rais Felix Tshisekedianatafuta muhula wake wa pili na wa mwisho wa miaka mitano, akishindana na majina mengine 26 kwenye kura. Mpinzani wake mkuu anaonekana kuwa Moise Katumbi, gavana wa zamani wa jimbo la Katanga na mfanyabiashara milionea ambaye kampeni yake mwaka 2018 ilizimwa na utawala uliopita wa Rais wa zamani Joseph Kabila.

Wakati akipiga kura mjini Lubumbashi, Katumbi aliwataka watu kusalia kwenye vituo vya kupigia kura na kufuatilia matokeo hadi mwisho. "Lazima tuhesabu kila kura na matokeo yaonyeshwe. Matokeo pekee ambayo tutayakubali yatakuwa yale yatakayoonyeshwa kwenye kila kituo," alisema.

DR Kongo | Uchaguzi Mkuu 2023 | Kituo cha kura Goma
Mamilioni ya Wakongo wanapiga Jumatano, Desemba 20, 2023, kuchagua rais, wabunge, magavana na wawakilishi wa manispaa.Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Bado, upinzani unaalia kugawanyika, na kumfanya Tshisekedi kuwa na nafasi kubwa ya kushinda. Mtoto huyo wa marehemu, kiongozi maarufu wa upinzani, ametumia muda mwingi wa urais wake kujaribu kuunganisha mamlaka juu ya taasisi za serikali na kufanya kazi ili kuondokana na mgogoro wa uhalali baada ya uchaguzi uliopingwa miaka mitano iliyopita.

"Ni mtu ambaye ameifanya mambo mengi nchi, amepigania demokrasia," alisema mfanyabiashara Joseph Tshabadi. Ingawa Tshisekedi hajafaulu kuzima ghasia mashariki, Tshibadi yuko tayari kumpa muda zaidi.

Soma pia: Wasifu wa Moise Katumbi

Tume ya uchaguzi inasema imefanya mabadiliko katika mchakato wa uchaguzi ili kuufanya uaminike zaidi, ikitumia zaidi ya dola bilioni moja kwa kura hiyo tangu mipango ilipoanza miaka miwili iliyopita. Mabadiliko muhimu kutoka 2018 ni kwamba matokeo kutoka kila mmoja kati ya vituo jumla 75,000 yatatolewa moja baada ya kiingine, badala ya kutangazwa kwa ujumla.

Matokeo yanapaswa kuwa ya mkono badala ya hesabu ya kielektroniki, alisema Mchungaji Eric Nsenga, mratibu wa misheni ya pamoja ya uangalizi wa uchaguzi kati ya Kanisa la Kristo la Kongo na Baraza la Maaskofu la Kitaifa la Kongo. Pia alionya dhidi ya kutoa hadharani matokeo ya sehemu yakiwa yanajumlishwa endapo yatachochea mvutano.

Wakimbizi wanapolilia haki yao ya kupiga kura huko Kongo.

Tayari baadhi ya waangalizi wamsema zoezi hilo halijakuw ana uwazi. Siku ya Jumatatu, Jumuiya ya Afrika Mashariki ilisema ujumbe wake wa waangalizi wa uchaguzi haukuruhusiwa kuingia Kongo na mamlaka. Mwezi uliopita, Umoja wa Ulaya ulifuta kazi yake ya uangalizi baada ya mamlaka ya Kongo kutoidhinisha matumizi ya vifaa vya satelaiti kwa ajili ya ujumbe wake.