1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongo imefikia wapi katika kupambana na rushwa ?

Jean-Noel Ba Mweze9 Desemba 2022

Mwendesha mashtaka mkuu ameomba kifungo cha miaka mitatu gerezani dhidi ya Vidiye Tshimanga, mshauri maalum wa zamani wa Rais Félix Tshisekedi aliyekuwa akihusika na masuala ya kimkakati.

https://p.dw.com/p/4KjQQ
Äthiopien Felix Tshisekedi Gipfeltreffen der Afrikanischen Union in Addis Abeba
Picha: Giscard Kusema/Press Office Presidency of DRC

Shitaka hilo, mwendesha mashtaka mkuu alilitamka hapo jana Alhamis wakati wa kesi kusikilizwa hadharani katika mahakama ya Gombe hapa mjini Kinshasa.

Mwanamikakati huyo wa zamani wa Rais Tshisekedi alishtakiwa baada ya kuonekana katika video akijadiliana kuhusu rushwa na wanaodaiwa kuwa wawekezaji katika sekta ya madini, akiwaahidi atajihusisha binafsi ili wapate kandarasi hiyo.

Vidiye Tshimanga alikana mashitaka na mawakili wake kutaja tofauti kadhaa katika hati ya mashtaka. Arthur Bomana ni mmoja wa mawakili wa Vidiye Tshimanga.

"Wale wanaodaiwa kuwa wawekezaji wa uongo, mwendesha mashitaka hakufanya jitihada za kuwatafuta hata huduma mbalimbali za serikali kuhusu shinikizo la madai kuwa watumishi wao walilazimishwa na mteja wetu. Tumetambua pia kukosekana uthibitisho wa ushahidi uliotumiwa na mwendesha mashtaka, yaani video zilizowekwa katika mitandao ya kijamii.", alielezea Bomana.

Hukumu inatarajiwa kutolewa mnamo Disemba 18. Lakini kesi ya Tshimanga siyo ya kwanza inayohusisha tuhuma za ufisadi kwa watu walio karibu na Rais Félix Tshisekedi aliyeingia madarakani kwa ahadi ya kuvifanya vita dhidi ya ufisadi kuwa mojawapo ya vipaumbele vyake.

Pato la taifa lawanufaisha viongozi waliowachache

Raia walio wengi hawajanufaika na pato la taifa
Raia walio wengi hawajanufaika na pato la taifaPicha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Baadhi ya jamaa zake waliopatikana na hatia ya ufisadi au ubadhirifu hatimaye waliachiliwa. Eteni Longondo, Waziri wa zamani wa Afya na mmoja wa viongozi wa UDPS, chama chake Rais Tshisekedi, aliyekamatwa Agosti 2021 kwa ubadhirifu wa zaidi ya dola milioni saba aliachiliwa siku chache baadaye, yaani Septemba 2021.

Huko Vital Kamerhe, kiongozi wa zamani wa ofisi ya Rais Tshisekedi, aliyepatikana na hatia mnamo Desemba 2020 kwa ufisadi na ubadhirifu wa zaidi ya Dola milioni 50, aliachiliwa mnamo Juni 2022.

Katika safu ya washirika wa Rais Tshisekedi, watu wengine bado wanashukiwa kuhusika, wakati ulimwengu ukiadhimisha leo Ijumaa, siku ya kimataifa dhidi ya ufisadi.

Swali linalohitaji suluhisho ya kisiasa, kama alivyoeleza Profesa Luzolo Bambi, mtaalamu wa mapambano dhidi ya rushwa.

"Rushwa ni jambo la kisiasa ambalo linahitaji suluhu la kisiasa. Rushwa inaharibu juhudi za serikali na juhudi za wananchi. Halafu mapambano dhidi yake yana manufaa kwani yanaruhusu bajeti ya serikali kuongezeka na hivyo kuiwezesha Serikali kukidhi mahitaji ya wananchi na ndivyo tunakuwa tukitambua",alisema Luzolo.

Ripoti ya Transparency International imeiweka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwenyi nafasi ya 169 miongoni mwa nchi 180 zilizo chini kabisa kwenye kupambana na ufisadi kwa mwaka 2021.