1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Kishida awasili Kyiv wakati Xi akikutana na Putin Moscow

Sylvia Mwehozi
21 Machi 2023

Rais wa China Xi Jinping amewasili Kremlin kwa mazungumzo rasmi na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin, wakati waziri mkuu wa Japan Fumio Kishida naye akiwasili mjini Kyiv kuonyesha mshikamano na Ukraine.

https://p.dw.com/p/4P1TK
Ukraine | Japans Premierminister Fumio Kishida in Bucha
Picha: Iori Sagisawa/AP/picture alliance

Waziri mkuu wa Japan Fumio Kishida amewasili mjini Kyiv mapema siku ya Jumanne kwa mkutano wake na Rais Volodymyr Zelenskiy katika ziara ya nadra ya kiongozi wa Japan ambayo haikutangazwa na kuonyesha msisitizo wa Tokyo katika kuisaidia Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi. Kishida alikuwa ndio kiongozi pekee katika kundi la nchi saba tajiri la G7 ambaye hakuwa ameitembelea Ukraine.

Mara baada ya kutua mjini Kyiv, Kishida ameutembelea mji wa Bucha, ambako vikosi vya Urusi vinatuhumiwa kwa mauaji ya watu wengi mwanzoni kabisa mwa uvamizi wake mnamo mwaka jana. Akiwa mjini Bucha, kiongozi huyo aliweka shada la maua nje ya kanisa kabla ya kukaa kimya kwa dakika chache.Waziri mkuu wa Japan aanza ziara ya ghafla Ukraine

Amesema kuwa "ulimwengu ulishangaa kuona mauaji ya raia wa Bucha wasio na hatia mwaka mmoja uliopita" na kuongeza kuwa Japan itaendeleza msaada wake kwa Ukraine katika juhudi za kurejesha amani. Japan inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele wa G7 mjini Hiroshima mnamo mwezi Mei. Hapo baadae waziri mkuu Kishida atakutana na kufanya mazungumzo na rais Zelensky.

Russlands Putin führt Gespräche mit Chinas Xi in Moskau
Xi na mwenyeji wake Putin mjini MoscowPicha: SERGEI KARPUKHIN/AFP

Wakati Kishida akiizuru Kyiv,  kwa upande wa pili, Rais wa China Xi Jinping naye tayari amewasili Kremlin kwa ajili ya kukutana na Rais Vladimir Putin katika duru ya pili ya mazungumzo rasmi mjini Moscow huku ajenda kubwa ikitarajiwa kuwa mzozo wa Ukraine. Xi aliingia Ikulu ya Kremlin kwenye zulia jekundu na kulakiwa na bendi ya kijeshi na ujumbe wa maafisa waandamaizi wa Urusi akiwemo Putin, huku mataifa yote mawili yakitafuta washirika ili kukabiliana na mataifa ya Magharibi.

Rais Xi apongeza uhusiano wa China na UrusiZiara ya kiongozi huyo wa China huko Moscow imetazamwa kama yenye kumtia nguvu Putin, ambaye yuko chini ya vikwazo vya nchi za Magharibi na chini ya waranti ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu juu ya tuhuma za kuwahamisha watoto wa Ukraine kinyume cha sheria.

Ikulu ya Kremlin ilisema viongozi hao wawili wangejadili mapendekezo yaliyotolewa na China ya kukomesha mapigano ya zaidi ya mwaka mmoja nchini Ukraine, na kwamba mazungumzo hayo huenda yakamalizika kwa Xi na Putin kutia saini msururu wa makubaliano. Awali, Xi alikutana na waziri mkuu wa Urusi Mikhail Mishustin na kuzisifu Urusi na China kama "madola mawili jirani yaliyo na nguvu" katika siku ya pili ya ziara yake. Xi alisema kuwa "Kuifanya Urusi kuwa eneo la kwanza la ziara ya viongozi wa China ni kutokana na mantiki ya kihistoria, kwa sababu sisi ni nchi kubwa jirani kwa kila mmoja. Sisi pia ni washirika wa kimkakati. Kwa miaka mingi, uhusiano wetu umestahimili jaribio la mabadiliko tofauti na kuwa thabiti kadiri muda unavyosonga"

Uhusiano wa kibiashara kati ya Beijing na Moscow umeimarika tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi huko Ukraine, ukiyaunganisha mataifa hayo kwa ukaribu zaidi na kuzua wasiwasi katika nchi za Magharibi kuhusu jinsi uhusiano huo utakavyokuwa. Xi, ambaye alisema kuwa amemwalika Putin kuzuru China mwaka huu, alisema serikali ya China "itaendelea kutoa kipaumbele kwa ushirikiano wa kimkakati wa pande zote kati ya China na Urusi".